Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
BENKI ya UBA Tanzania imezindua mfumo wa malipo wa Pan-African Payment and Settlement System (PAPSS), unaolenga kurahisisha miamala ya kuvuka mipaka kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wateja kutuma na kupokea fedha katika nchi za Afrika zinazoshiriki mfumo huo kwa kutumia sarafu za nchi zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Flavia Kiyanga, Mkuu wa Idara ya Huduma za Uendeshaji wa UBA Tanzania, amesema mfumo huo utarahisisha malipo ya kimataifa kwa kuondoa mlolongo mrefu wa benki wakilishi uliokuwa ukitumika katika kutuma fedha baina ya nchi.
“PAPSS inakuja kurahisisha wafanyabiashara kufanya malipo. Mlolongo wa zamani ulihusisha kupitia benki wakilishi kabla fedha hazijamfikia mpokeaji, lakini kupitia PAPSS, fedha zinaweza kufika kwa wakati baada ya muamala kukamilika,” amesema Kiyanga.
Amesema mfumo huo utawawezesha wafanyabiashara kutumia akaunti zao za shilingi za Tanzania kufanya malipo katika nchi nyingine zinazoshiriki PAPSS, hatua itakayopunguza muda wa miamala na kurahisisha biashara baina ya nchi za Afrika.
Kiyanga ameongeza kuwa UBA imeamua kujiunga na mfumo huo kutokana na kukua kwa shughuli za biashara nchini Tanzania, huku akiishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zinazochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Juma Kalumwana, Msimamizi wa Huduma za Malipo ya Kitaifa wa UBA Tanzania, amesema wateja wanaweza kutumia mfumo huo kupitia matawi ya benki au njia za kidijitali zinazopatikana kupitia WhatsApp na Facebook.
“Huduma ya PAPSS kupitia WhatsApp na Facebook inalenga kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za kifedha, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya simu janja nchini Tanzania,” amesema Kalumwana.
Amefafanua kuwa huduma hiyo itawawezesha wateja kufanya miamala kupitia simu zao bila kulazimika kutembelea matawi ya benki. Kwa wateja wanaotembelea matawi, wanapaswa kuwa na taarifa za mpokeaji, ikiwemo namba ya akaunti na kiasi cha fedha wanachotaka kutuma.
Kalumwana amesema gharama za kutuma fedha kupitia PAPSS ni asilimia 2.5 ya kiasi kinachotumwa, huku tozo ya juu ikiwa dola 20 za Marekani, sawa na takribani Shilingi 70,000 za Tanzania.
Kuhusu vikomo vya miamala, amesema mteja anaweza kutuma hadi dola 5,000 kwa muamala mmoja na dola 10,000 kwa siku, kulingana na masharti ya huduma na kiwango cha ubadilishaji fedha cha siku husika.
Ameongeza kuwa mfumo huo unazingatia usalama wa miamala yote ya kifedha, Pia, mtumaji anatakiwa kuwa na akaunti ya UBA, lakini mpokeaji anaweza kupokea fedha kupitia benki nyingine zinazoshiriki mfumo wa PAPSS bila kuwa na akaunti ya UBA.

Naye Geofrey Magugi, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa UBA Tanzania, amesema benki hiyo imekuwa ya kwanza nchini kuingia makubaliano na mfumo wa PAPSS kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za kifedha na kurahisisha biashara barani Afrika.
“Kujiunga na mfumo wa PAPSS ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za kifedha na kurahisisha malipo ya kuvuka mipaka, huku wafanyabiashara wakipata fursa ya kufanya miamala kwa urahisi zaidi katika nchi za Afrika zinazoshiriki mfumo huo,” amesema Magugi.

More Stories
Mtandao walaani mauaji ya Wanawake, Wasichana nchini
Ndejembi:Mradi wa TAZA kuchochea Maendeleo
Afrika yatathmini mikakati ya kuimarisha usafiri wa majini