October 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwigulu :Nchi za Afrika imarisheni usafiri wa majini

Na Penina Malundo,TimesMajira

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano na kuwekeza katika usafiri wa majini ili kukuza biashara ya kikanda, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje ya bara hilo.

Amesema kuunganisha bandari na miundombinu ya reli na barabara kutasaidia kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria, kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumza leo  jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Masuala ya Usafiri wa Majini kwa Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA), Dkt. Nchemba alisema janga la UVIKO-19 na migogoro ya kimataifa vimeonesha umuhimu wa Afrika kujenga mifumo imara ya usafirishaji na biashara.

Amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika meli, kuimarisha kampuni za usafirishaji za kikanda na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi ili kuwezesha bidhaa kusafirishwa kwa ufanisi kati ya bandari za nchi wanachama.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kikanda kupitia mafunzo ya wataalamu na maandalizi ya chuo cha kikanda cha usafirishaji wa majini.

Amesema hatua hizo zitasaidia kuongeza ujuzi, kuboresha uwezo wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza usalama wa shughuli za usafiri wa majini.