October 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kujenga Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Kanda

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

TANZANIA imeeleza utayari wa kushirikiana na nchi wanachama wa Baraza la Mawaziri la Kanda ya Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOESNA) katika kuanzisha chuo kikuu cha kikanda kitakachojikita katika elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu wa sekta ya usafiri wa majini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema uamuzi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa Afrika katika sekta ya usafiri wa majini.

Kihenzile amesema Tanzania pia itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa MOESNA utakaofanyika Oktoba 15, 2026 jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha mawaziri 26 wanaosimamia uchukuzi na lojistiki kutoka nchi wanachama.

Amesema mkutano huo utajadili namna ya kuimarisha uunganishaji wa nchi, kurahisisha biashara na kuongeza usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya maji kati ya bandari za Afrika, huku ukilenga kuongeza ushiriki wa bara katika usafirishaji wa majini.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa MOESNA, Kassim Mpaata, amesema tayari wamepata ushirikiano kutoka Tanzania, Botswana na nchi nyingine katika kufanikisha ujenzi wa chuo hicho, ambacho kinatarajiwa kuwa kituo cha umahiri wa kikanda katika sekta ya usafiri wa majini.