
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Waziri mkuu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt,Mwigulu Nchemba amezitaka familia kuwa na mpango wa kukabiliana na maafa kabla hayajatokea ili kuzijengea uwezo wa kukabiliana nayo pindi yanapotokea.
Hayo ameyasema leo Oktoba 13 mjini Sumbawanga Kwenye uwanja wa Nelson Mandela kama kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupunguza maafa ambapo amedai kuwa ili kuweza kukabiliana na maafa ni lazima mipango hiyo ikaanzia katika ngazi ya familia.
Alisema kuwa wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na majanga ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya mbalimbali ya maafa upo umuhimu mkubwa wa jamii kuanzia ngazi ya familia kuwa na mikakati ya kukabiliana na maafa kabla na baada ya kutokea.

Dkt, Nchemba amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Ustahimilivu unaanzia nyumbani”na kuwa hiyo inatukumbusha namna ambavyo jamii zetu zimekuwa zikipitia madhira makubwa kupitia maafa mbalimbali licha ya kuwaachia makovu yasiyosahaulika.
Waziri mkuu huyo alifafanua kuwa mbinu za kukabiliana na maafa kulingana na mazingira yetu jamii husika inalo jukumu la kuhakikisha wanapewa mbinu za kisasa ikiwa ni pamoja na zile za jadi na kuwa hiyo itasaidia kupunguza ukubwa wa majanga pale yanapotokea kwa maana jamii husika itakuwa imekabiliana nayo kwa kiasi kikubwa.
Siku ya kimataifa ya kupunguza maafa iliaasisiwa mwaka 1989 kama njia ya kupunguza vihatarishi vya maafa duniani ambavyo vimekuwa vikiacha huzuni kwa watu
Alidai kuwa suala la mabadiliko ya tabia ya Nchi ni moja ya visababishi vya maafa mbalimbali na kuwa jamii na Serikali kwa ujumla wanalo jukumu la kuimarisha mapambano ya uharibifu wa mazingira kwa kuhakikisha jamii kwa ujumla inauelewa mkubwa juu ya mabadiliko hayo na namna ya utatuzi wake.
Akitolea mifano mbalimbali ya maafa ambayo Watanzania wameyapitia ni pamoja na maporomoko ya Hanang na Mbeya, Mafuriko na ajali ambazo zimewaacha Watanzania wengi na majonzi makubwa.

Pia waziri Mkuu ameitumia Fursa hiyo kupata taarifa ya maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge wa uhuru ikiwa ni pamoja na wiki la vijana ambapo waziri wa maendeleo ya vijana Joel Nanauka alieleza maandalizi kwa ujumla yamefikia asilimia 100 huku wiki la vijana likitumika vizuri kuwajenga vijana kuwa wajasiri na kuzitambua fursa

More Stories
NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji.
Mbozi kuibadili stendi ya Malori kuwa Kariakoo.
HESLB yavunja rekodi, yakusanya bilioni 235.5/-