October 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yaeleza sababu kutangaza bei za mafuta

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIKA mazingira ya sasa, ambapo bei za bidhaa za mafuta katika soko la Dunia zinabadilika kutokana na migogoro ya kimataifa,gharama za usafirishaji na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, usimamizi wa bei una umuhimu katika kulinda maslahi ya wananchi na uchumi wa Taifa.

Nchini Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ina jukumu la kusimamia bei katika sekta inazozidhibiti kwa mujibu wa sheria.

Katika sekta ndogo ya mafuta, EWURA hutangaza bei kikomo za petroli, dizeli na mafuta ya taa ili kuhakikisha kuwa bei zinazotozwa zinazingatia gharama halisi na utaratibu wa udhibiti uliowekwa.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Salum Mnuna ameeleza sababu na lengo la mamlaka hiyo kutangaza bei si kufanya mafuta yawe na bei ya juu, bali kuhakikisha bei zinazotozwa ni za haki, zinazingatia mwenendo wa soko na kulinda maslahi ya watumiaji pamoja na watoa huduma.

Mnuna amesema,katika kupanga bei kikomo za mafuta, EWURA huzingatia gharama mbalimbali, zikiwemo bei za ununuzi katika soko la dunia, usafirishaji, bima, viwango vya ubadilishaji fedha, kodi, tozo na gharama nyingine zinazotambuliwa katika mfumo wa ukokotoaji wa bei.

Amesema,kwanza, bei kikomo humlinda mwananchi dhidi ya kutozwa bei zinazozidi kiwango kilichoidhinishwa,hivyo husaidia kuzuia baadhi ya wafanyabiashara kutumia mabadiliko ya soko kuongeza bei kiholela.

Pili, utangazaji wa bei huongeza uwazi kwani mwananchi anaweza kujua bei inayopaswa kutozwa katika eneo lake na hivyo kuwa na msingi wa kudai haki yake anaponunua mafuta.

Tatu, usimamizi wa bei husaidia kuweka uwiano kati ya maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara, ili wananchi wapate bidhaa kwa bei zinazozingatia gharama huku biashara zikiendelea kuwa endelevu.

Pia amesema,mafuta ni bidhaa muhimu katika shughuli za uchumi,humika katika usafirishaji wa abiria na mizigo, kilimo, viwanda na utoaji wa huduma mbalimbali.Hivyo usimamizi wa bei unaozingatia gharama na uwazi husaidia biashara kupanga matumizi, kupunguza uwezekano wa utozaji wa bei holela na kuongeza utabirika wa gharama katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, mfumo wa bei unaotabirika na unaozingatia gharama unaweza kusaidia kudumisha ushindani wa haki, kulinda uwekezaji na kuwezesha upatikanaji endelevu wa bidhaa za mafuta nchini.

Hata hivyo amesema,kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya mabadiliko ya bei za mafuta duniani, kutokuwepo kwa bei kikomo na mfumo madhubuti wa usimamizi kunaweza kuongeza hatari ya baadhi ya wafanyabiashara kutoza bei kubwa zisizoendana na gharama halisi.

Hali hiyo inaweza kuongeza gharama za usafirishaji, uzalishaji na maisha ya wananchi pia kupunguza uwazi wa bei na kufanya iwe vigumu kwa watumiaji kutambua iwapo wanatozwa bei inayostahili.