October 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ‘Ongea na Kamanda’ yazinduliwa Mwanza

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza 

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa, amezindua kampeni ya ‘Ongea na Kamanda’ inayolenga kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya jeshi hilo na wananchi katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na kudumisha amani na utulivu.

Kupitia kampeni hiyo, wananchi wamepata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na Kamanda wa Polisi, kueleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kutoa maoni kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa kuboresha usalama.

Akizungumza na wananchi katika stendi ya mabasi ya Nyegezi Oktoba 10,2026 DCP. Mutafungwa amesisitiza umuhimu wa kusikiliza maoni ya wananchi wakiwemo madereva,abiria na wafanyabiashara, kuhusu masuala ya usalama yanayowagusa katika shughuli zao za kila siku.

Ameeleza kuwa maoni na changamoto zitakazokuwa zinawasilishwa kupitia mikutano ya hadhara zitapokelewa na kufanyiwa kazi kwa lengo la kuimarisha usalama na kuboresha mazingira ya wananchi katika maeneo yao.

Aidha, kampeni hiyo inalenga kuwapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto zinazohusu usalama barabarani, ikiwemo masuala yanayowakabili madereva na abiria pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya stendi.

Kwa upande wake,Katibu wa UWT Kata ya Nyegezi Safia Mohamed,amepongeza huduma nzuri ya polisi inayotolewa katika Kituo cha Polisi Nyegezi.

“Ulinzi katika kata yetu umeimarika vizuri. Afande Mrema alitununulia vifaa vya ulinzi shirikishi, kwa kweli Mungu ambariki sana,”amesema Mohamed.

Naye Salehe Othman,amempongeza Mkaguzi wa Kata ya Nyegezi, Insp. Abdallah Mrema, kwa kuviwezesha vikundi vya ulinzi shirikishi na kuvipatia vifaa kwa ajili ya kutimiza majukumu yao jambo lililofanya kata hiyo kuendelea kuwa na utulivu.