Na Mwandishi Wetu,Mbeya
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuwawezesha wataalamu wa Kitanzania kutatua changamoto za wananchi na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Prof. Mkenda ameyasema hayo mkoani Mbeya wakati wa ziara yake katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya chuo kupitia Mradi wa HEET, kutembelea bunifu zinazofanywa na wanafunzi na watafiti pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa chuo.
Amesema vyuo vya sayansi na teknolojia vinapaswa kuelekeza nguvu katika tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto halisi za wananchi, huku kukiwa na mazingira yatakayowezesha bunifu hizo kukua na kutumika katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Prof. Mkenda amesema ni muhimu vyuo kama MUST, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Nelson Mandela African Institute of Science and Technology kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kubuni na kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa, ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.
“Baada ya miaka 133 tangu reli ya kwanza ijengwe, bado tunapoamua kujenga reli tunatafuta watu kutoka nje. Lazima tujiulize, kwa nini tusiamini uwezo wa wahandisi wetu?” amesema Prof. Mkenda.
Akisisitiza umuhimu wa kujiamini na kutumia uwezo wa wataalamu wa ndani, Prof. Mkenda amerejea kauli ya marehemu Reginald Mengi, “Yes, we can, we will, we must,” akisema Watanzania wanapaswa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kutegemea zaidi utaalamu kutoka nje.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu, hususan vijana, ili bunifu zao ziweze kuendelezwa hadi kufikia hatua ya kuzalisha bidhaa na huduma zinazotumika nchini na kuuzwa katika masoko ya nje.
Prof. Mkenda amewapongeza wabunifu wa MUST kwa kuibua teknolojia mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za jamii, akieleza kuwa uwekezaji katika ubunifu unaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa ndani, kutengeneza ajira, kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

More Stories
CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi
VETA yafungua milango ya mafanikio kwa wenye ulemavu
Zungu: Tanzania ipo tayari kuchangia uzoefu huduma mama , mtoto