Na Joyce Kasiki, Rukwa
MAFUNZO ya ufundi stadi kupitia vyuo vya VETA nchini yanaendelea kuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi, huku wanafunzi wenye ulemavu wakipata fursa ya kuonesha uwezo wao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Miongoni mwa vijana wanaonufaika na fursa hiyo ni Imelda Kanyengele, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea ushonaji katika Chuo cha VETA Nkasi mkoani Rukwa, ambaye amesema mafunzo anayopata yamemjengea ujuzi na kuongeza uwezo wake wa kujiajiri.
Akizungumza Oktoba 9, 2026, wakati wa Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yenye kaulimbiu “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” Imelda amesema kwa sasa ana uwezo wa kushona aina mbalimbali za mavazi, yakiwemo suruali, mashati na magauni, pamoja na kutengeneza batiki.
Amesema kabla ya kujiunga na mafunzo hayo hakutarajia kufikia kiwango cha ujuzi alichonacho sasa, lakini juhudi zake pamoja na maelekezo kutoka kwa walimu vimemsaidia kuimarika katika fani hiyo.
Imelda amewashukuru walimu wake kwa kumfundisha na kumsimamia katika kipindi chote cha mafunzo, akieleza kuwa ujuzi huo umempa nafasi ya kuhudumia wateja wa rika mbalimbali wenye mahitaji tofauti ya mavazi.
Aidha, amewahimiza vijana wenzake, hususan wenye ulemavu, kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi zilizopo nchini badala ya kukata tamaa kutokana na changamoto wanazokutana nazo.
Amesisitiza kuwa vijana wenye ulemavu wana uwezo wa kujifunza, kukuza vipaji vyao na kujenga maisha ya kujitegemea wanapopewa nafasi na kutumia fursa zinazopatikana.
Mwisho.

More Stories
CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi
Mkenda: Tuamini wataalamu wetu, tupunguze utegemezi wa Nje
Zungu: Tanzania ipo tayari kuchangia uzoefu huduma mama , mtoto