Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Korogwe
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira HTM – Korogwe wametekeleza jitihada za kufungua huduma ya maji kwenye vijiji vinane na kitongoji kimoja wilayani Handeni, na vitongoji viwili katika Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Vijiji na vitongoji hivyo vilikosa maji kwa vipindi virefu kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitano kwa baadhi ya vijiji. Jitihada za HTM WSSA zimewezesha kupatikana kwa huduma hiyo katika kipindi cha muda mfupi.

Hayo yamesemwa kwenye taarifa iliyotolewa na Menejimenti ya HTM WSSA Oktoba 9, 2026 iliyowasilishwa kwa waandishi wa habari.
Taarifa hiyo inasema nia ya Serikali ni kuona wananchi wote wanapata maji ya kutosha, na hivyo HTM WSAA itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kufufua huduma kwenye vijiji vyote vilivyokuwa vinahudumiwa na maji na Mradi wa HTM uliojengwa mwaka 1974 na zilizokuwa Mamlaka za Maji za Handeni, Korogwe na Mombo.
Taarifa hiyo pia imeonesha kuwa matarajio ya Menejimenti ni kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayohudumiwa na HTM WSSA yanapata huduma ya kuaminika hasa baada ya kukamilika kwa Mradi Mkubwa wa Miji 28 unaotarajiwa kunufaisha wakazi wa Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, pamoja na vijiji vinavyopitiwa karibu na bomba kuu.
Taarifa hiyo ilivitaja vijiji na vitongoji anbavyo kwa muda mrefu vilikosa huduma ya maji, na sasa vinapata maji kuwa ni Magamba kilichopo Kata ya Magamba, Kweditilibe na Kwedibangala, Kata ya Kiva, Nkale, Kata ya Kwamatuku, Komdudu, Kata ya Kwamkono, Mzundu, Kata ya Ndola kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Kwa Halmashauri ya Mji Handeni, maji yamefika Kitongoji cha Mji Mpya, Kata ya Kwamagome, Mtaa wa Msasa, na Kwemgodi, Kata ya Msasa. Kwa upande wa Wilaya ya Korogwe ni vitongoji vya Jitengeni na Mwisho wa Shamba, Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo.


More Stories
Mkenda: Tuamini wataalamu wetu, tupunguze utegemezi wa Nje
VETA yafungua milango ya mafanikio kwa wenye ulemavu
Zungu: Tanzania ipo tayari kuchangia uzoefu huduma mama , mtoto