Na Penina Malundo,TimesMajira
RAIS mpya wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi la Australia Milton Dick ameahidi kuimarisha umoja, demokrasia na ushirikiano miongoni mwa mabunge ya nchi wanachama, akisema atahakikisha sauti za mataifa yote zinasikilizwa bila kujali ukubwa au uwezo wake wa kiuchumi
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa IPU kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2029, uliofanyika leo Oktoba 9, 2026 katika kikao kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Rais huyo amesema kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa 32 wa taasisi hiyo ni heshima kubwa zaidi katika maisha yake.
Amesema hatasahau imani aliyopewa na wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya kijiografia na kisiasa, maeneo tofauti na pembe zote za dunia, akitoa shukrani kwa wote waliounga mkono azma yake pamoja na wale waliowaunga mkono wagombea wengine.
“Leo hakuna washindi wala walioshindwa. Leo IPU imezungumza kwa sauti moja. Hii ndiyo demokrasia na ni ukumbusho kwamba mazungumzo, kuheshimiana na ushirikiano bado vina umuhimu,”amesema.
Amesisitiza kuwa uongozi wake utazingatia mshikamano na kutafuta maeneo ya pamoja kati ya mataifa, akieleza kuwa mambo yanayowaunganisha watu ni makubwa zaidi kuliko yale yanayowatenganisha.
Aidha, ameahidi kutetea maslahi ya mataifa madogo na kuhakikisha yanapata nafasi ya kusikilizwa katika majukwaa ya kimataifa, huku akieleza kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inahitaji ushirikiano wa dunia nzima.
Rais huyo mteule amesema ataanza kutekeleza majukumu yake mara moja kupitia mpango wa siku 100 za kwanza, akiahidi kuongoza kwa unyenyekevu, uadilifu na kuheshimu maoni ya wengine.
Amesema dunia inawategemea wabunge katika kutetea Demokrasia, kuimarisha amani, kulinda uhuru na kujenga mustakabali bora kwa vizazi vijavyo, akitoa wito kwa wanachama wa IPU kushirikiana kujenga Demokrasia yenye manufaa kwa watu wote duniani.

More Stories
Milton Dick Rais Mpya wa IPU
TANESCO yang’ara tuzo ya mawasiliano
Wiki ya vijana yageuka kitovu Cha fursa na ubunifu:Rukwa