–Lengo ni kukabiliana na ongezeko la wanafunzi 120 ‘Double Cohort’ 2028, Mpemba Sekondari

Na Moses Ng’wat, Tunduma
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari Mpemba, Halmashauri ya Mji Tunduma.
Ujenzi huo unalenga kuongeza nafasi za madarasa ili shule hiyo iwe tayari kupokea wanafunzi wapya 120 watakaotokana na kundi la wanafunzi wa darasa la sita na la saba wanaotarajiwa kuhitimu kwa pamoja mwaka 2027, maarufu kama Double Cohort.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi na kupanda mti katika eneo la shule hiyo, Mwang’onda amesisitiza mambo mawili, ambapo amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule.
Pia kiongozi huyo wa Mwenge, ametoa msisitizo kwa wanafunzi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu inayojengwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo, iliyosomwa na Mkuu wa shule hiyo, Furaha Mhagama kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, ujenzi huo unagharimu Sh mil 75 na ulianza Agosti 9, 2026, huku ukitarajiwa kukamilika Novemba 9, mwaka huu.

Mradi huo umewekewa jiwe la msingi ukiwa miongoni mwa miradi 44 ya ujenzi wa vyumba vya madarasa inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji Tunduma kwenye shule za sekondari 13, kwa lengo la kuongeza miundombinu ya elimu kabla ya kuwasili kwa kundi hilo la wanafunzi.
Hadi sasa, Sh milioni 58.02 zimetumika katika malipo ya mafundi na ununuzi wa vifaa vya ujenzi, huku Sh milioni 16.97 zikiwa zimesalia kwa ajili ya kukamilisha mradi huu unaojengwa kwa mfumo wa Force Account.



More Stories
Sekam :Serikali zitunze haki za Wafanyakazi katika enzi ya AI
Bunge lipo tayari kushirikiana na Mabunge mengine
TADB yatoa tuzo kwa wanafunzi 13 SUA