October 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zungu achaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU


Na Penina Malundo,TimesMajira


SPIKA wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.


Akizungumza baada ya kuchaguliwa nafasi hiyo leo jijini Arusha, Zungu amesema nafasi hiyo inaongeza heshima ya Tanzania katika diplomasia ya kibunge kimataifa na kutoa fursa ya kuimarisha uhusiano na mabunge ya nchi mbalimbali.


Amesema mkutano huo pia umefungua fursa za kiuchumi kwa Tanzania, hususan Arusha, kutokana na ujio wa wajumbe kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao wamepata nafasi ya kuona vivutio, bidhaa na fursa zinazopatikana nchini.


Zungu amewataka Watanzania kutumia fursa zinazotokana na mkutano huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiajiri.


Aidha, amesema Bunge lina wajibu wa kusimamia Serikali na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa, akisisitiza kuwa Bunge ni chombo cha wananchi na si cha watu wachache.


Mkutano huo unawakutanisha wabunge kutoka mabunge wanachama duniani kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utawala bora, ushirikishwaji, uaminifu na fursa kwa wote.