Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Dar
WAZIRI wa Fedha,Balozi Khamis Omar, amesema Tanzania inachangia takribani asilimia 0.31 ya uzalishaji wa gesi joto duniani, lakini inakabiliwa na athari kubwa za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kushuka kwa uzalishaji wa mazao na uharibifu wa miundombinu.
Balozi Omar amesema hayo jijini Dar-es- Salaam wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano Kuhusu Upatikanaji wa Fedha za Ufadhili wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2026 (Tanzania Climate Finance Roundtable), uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) chini ya kaulimbiu “Unlocking Climate Finance in the United Republic of Tanzania.”

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa Serikali,washirika wa maendeleo, taasisi za fedha na sekta binafsi, huku Balozi Omar akisema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuongeza mahitaji ya rasilimali za fedha kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko hayo.
Amesema kupitia Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) Toleo la Pili (NDC 2.0), Tanzania inahitaji takribani dola za Marekani bilioni 19.3 kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za tabianchi, huku ikikabiliwa na pengo la fedha linalokadiriwa kufikia dola bilioni 12.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa amesema, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatarajia Tanzania kuwa na watu takribani milioni 118 na uchumi unaokaribia dola trilioni moja, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa mazingira yatakayowezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa uendelevu.
Amesema,miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele ni uhifadhi wa vyanzo vya maji, upandaji na utunzaji wa misitu pamoja na udhibiti wa taka, ikiwemo taka ngumu, plastiki na maji machafu yenye kemikali yanayoweza kuishia baharini.
Aidha, Kwagilwa amesema,hatua hizo ni muhimu katika kulinda mazingira wakati idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zikiongezeka.
Pia amesema,Serikali inalenga kuongeza uwekezaji katika shughuli endelevu na zinazolinda mazingira sambamba na kuimarisha hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kutumia fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.



More Stories
Ndile atoa msisitizo matumizi sahihi fedha za Serikali
Vijana Rukwa wahamasishwa kushiriki wiki la vijana
Tanzania mwenyeji mkutano wa COP12