
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
MKUU wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Mohamed Mtulyakwaku amesema kuwa suala la amani na usalama litapewa kipaumbele na kuanzisha kampeni ya mjue jirani yako kama njia ya kuhakikisha suala la amani linakuwepo kwa Wananchi.
Hayo alisema Jana Oktoba 3,2026 kwenye kikao kilichowajumuisha Watu wa makundi mbalimbali wakiwemo Wazee katika kikao chake cha kwanza cha kujitambulisha kwa Wananchi tangu ahamishiwe wilayani Nkasi akitokea wilayani Kaliua mkoani Tabora
Alisema kuwa amani ndiyo msingi wa Kila kitu na kuwaomba Wazee wasimamie suala la maadili na malezi kwa Watoto wao kwani wakilelewa katika misingi yenye maadili hata vitendo vya kihalifu vitapungua sana kama siyo kumalizika kabisa

Mtulyakwaku amewataka Wazee kuwafichua vijana wao ambao ni wahalifu kwa Kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola na kuwa suala la amani atalisimamia ipasavyo kwa kuhakikisha wahalifu wote wanashughulikiwa ipasavyo ili jamii iweze kuishi kwa amani.
Sambamba na hilo pia amewataka Wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za Elnino zinazotarajia kuanza wakati wowote kuanzia Sasa kwa kuhama maeneo hatarishi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa kufuata maelekezo ya wataalamu kama wanavyoelekeza.
Alidai kuwa Serikali imejitahidi kuielimisha jamii juu ya athari zitokanazo na mvua hizo za Elnino hivyo ni jukumu la Kila mmoja kuchukua tahadhari juu ya mvua hizo ili kujihakikishia usalama wa Kila mmoja katika kipindi chote cha mvua za El Nino

Pia aliwataka wazazi kuendelea kuwapeleka Watoto wao shule ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata chakula shuleni ili kuwajengea afya na hakiri ili waweze kupata elimu itayowasaidia katika maisha Yao,huku akisisitiza umuhimu wa elimu kwa Watoto.
Katika mkutano huo pia aliruhusu Wazee Kutoa hoja ambapo walimweleza mambo mbalimbali yaliyogusa sekta mbalimbali ikiwemo afya,maji na ardhi ambapo aliziagiza sekta husika kushughulikia kero zilibainishwa haraka ambapo nyingi zilipewa muda wa wiki mbili ziwe zimeshughulikiwa.
Kwa upande RUWASA NA NAUWASA wameagizwa kuwasiliana na Watu wa bonde ili waweze kufanya utafiti maji kwa kubaini maeneo yenye maji kiasili kwa kushirikiana na Wananchi ili waweze kuweka mikakati madhubuti ya kuchimba visima vitakavyopunguza tatizo la maji kwa Wananchi

More Stories
Warda akabidhiwa rasmi ofisi Kibaha
TUWASA yaboresha utoaji huduma
Ndejembi apeleka ujumbe wa Tanzania Afrika