October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GF yakabidhi magari kwa wachimbaji, yaongeza huduma


Na Joyce Kasiki, Geita

KAMPUNI ya GF Trucks & Equipment imetumia Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mjini Geita kuwaunganisha wachimbaji na wadau wa sekta ya madini na teknolojia za usafirishaji, huku ikikabidhi magari kwa baadhi ya wateja wake.


Akizungumza katika maonyesho hayo, Meneja wa Biashara na Masoko wa GF Trucks & Equipment, Smart Deus, alisema kampuni hiyo imefanikiwa kukabidhi magari kwa wateja wake katika maonyesho hayo, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya usafirishaji kwa shughuli za uchimbaji madini.


Deus amesema kampuni hiyo pia ina kiwanda cha kuunganisha magari kinachofanya kazi kupitia GF Vehicle Assemblers, kilichopo Kibaha mkoani Pwani.


Amesema uwepo wa kampuni hiyo katika maonyesho ya Geita ni sehemu ya kuendelea kuwafikia wadau wa sekta ya madini na kuwapatia taarifa kuhusu bidhaa na huduma wanazotoa.


“Tunawapongeza waandaaji wa maonyesho haya na tunawakaribisha Watanzania pamoja na wachimbaji kutembelea banda letu ili kupata fursa ya kufahamu zaidi kuhusu bidhaa na huduma tunazotoa,” amesema Deus.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Amotech Mine Services, Joffrey Mwaselera, amesema kampuni yake imepata fursa ya kununua na kukabidhiwa gari aina ya Mahindra katika viwanja vya maonyesho hayo.


Mwaselera amesema Amotech Mine Services inatoa huduma mbalimbali katika sekta ya madini, ikiwamo uchorongaji, usafirishaji na uchimbaji wa madini.


Amesema ushirikiano wao na GF Trucks & Equipment umekuwa muhimu katika kupata magari na vifaa vinavyosaidia utekelezaji wa shughuli zao za uchimbaji.


Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwamo kampuni zinazotoa teknolojia, vifaa na huduma kwa wachimbaji na kampuni za uchimbaji madini.