Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
DAKTARI Bingwa Bobezi wa Moyo wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt.Ernest Elisenguu, amewataka Watanzania kuacha matumizi ya sigara na bidhaa nyingine za tumbaku pamoja na pombe akisisitiza kuwa hakuna kiwango cha matumizi kinachoweza kutajwa kuwa salama katika kuzuia magonjwa ya moyo.
Amesema,sigara na bidhaa za tumbaku,ugoro na shisha si kitu cha kupunguza matumizi, bali ni cha kuacha, huku akionya kuwa moshi wake unaweza kuwaathiri hata watu ambao hawavuti.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani ambayo ufanyika kila Septemba 29 ya kila mwaka,ambapo hospitali hiyo iliungana na Dunia katika kuadhimisha Siku hiyo,Dkt.Elisenguu pia amewataka Watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 40 kuanza kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo hata kama hawana dalili.
Hatua hiyo ni muhimu katika kubaini mapema matatizo ya moyo na kuzuia gharama kubwa za matibabu, akisisitiza kaulimbiu ya mwaka huu ni “usipoteze mapigo”,kwani Watanzania wengi wana tabia ya kusubiri hadi wapate dalili ndipo waende hospitali, wakati baadhi ya dalili za awali za magonjwa ya moyo zinaweza kutotiliwa maanani.
“Ili tuwagundue hawa watu mapema, wenye hiyo miaka inabidi waanze kwenda hospitali ili kupima shinikizo la damu,sukari,mapigo ya moyo,mafuta kwenye mwili na damu, akishafanya vile tunamfanyia vipimo vya moyo,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Elisenguu, uchunguzi wa awali huanza kwa mtu kukutana na Daktari wa Moyo ili kubaini kama ana dalili, na kwa wale wasiokuwa na dalili kuna vipimo vinavyoweza kufanyika mapema, ikiwemo ECG na ECHO. Alisema vipimo hivyo vinaweza kusaidia kubaini kama mtu ana dalili au ugonjwa wowote wa moyo kabla hali haijawa kubwa.
Amesema magonjwa mengi ya moyo yanaweza kuzuilika, huku gharama kubwa zikiwa katika matibabu.Magonjwa hayo huwapata watoto na watu wazima, ambapo kwa watoto baadhi hutokana na kurithi au kuzaliwa wakiwa na matatizo hayo, wakati kwa watu wazima vyanzo ni vingi, huku shinikizo la damu likiwa miongoni mwa sababu kubwa.
“Kwa Tanzania, asilimia zaidi ya 40 wanasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu,ni muhimu wa wananchi kufahamu viashiria vya afya zao.Wizara ya Afya imekuwa ikihimiza wananchi kujua namba zao ikiwemo namba ya kawaida ya shinikizo la damu, mapigo ya moyo, sukari, uzito na uwiano wa urefu na uzito,”.
Dkt.Elisenguu amesema,kuna uhusiano mkubwa kati ya lishe na magonjwa ya moyo, akieleza kuwa shinikizo la damu lina uhusiano na mfumo wa maisha,aliwashauri Watanzania kupunguza vyakula vya wanga, nyama nyekundu na matumizi ya chumvi nyingi, huku wakitumia zaidi mboga za majani na matunda. Alisisitiza kuwa si kwamba vyakula hivyo havifai, bali matumizi yake kwa wingi yanaweza kuwa na madhara.

Pia amewataka Watanzania kufanya mazoezi angalau dakika 150 kwa wiki, akisema mtu anaweza kutenga nusu saa kila siku kwa ajili ya mazoezi, ikiwemo kutembea kwa mwendo wa kasi bila kuhitaji vifaa maalumu.
Dkt. Elisenguu amesema magonjwa ya moyo ni ya aina nyingi na mengi yanatibika hapa nchini, ambapo takribani asilimia 98 ya magonjwa hayo yanatibika Tanzania, huku machache yakihitaji wagonjwa kupelekwa nje ya nchi,hivyo alisisitiza kuwa kuzuia magonjwa hayo mapema kutasaidia kupunguza gharama za matibabu endelevu na ufuatiliaji kwa wagonjwa pamoja na kupunguza mzigo wa Serikali katika kugharamia matibabu.
Kwa upande wake, Neema Mwita, mmoja wa wananchi waliojitokeza kupima afya ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, ameiomba Serikali kuongeza juhudi za kupiga vita uzalishaji wa sigara na pombe, akisema matumizi ya vitu hivyo ni hatari kwa afya na vijana wengi wamekuwa waathirika.

More Stories
Umoja Afya ya NHIF yawavutia wengi Geita
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba
Nzilanyingi ashauri jiji kukopa kuboresha barabara