September 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bura awataka wananchi kulinda Miundombinu, kutumia nishati safi



Na Joyce Kasiki, Geita


MKUU wa Wilaya ya Chato, Luis Bura, amewataka wananchi kushirikiana na taasisi zinazohusika na huduma za nishati kutoa taarifa kuhusu changamoto za umeme na kulinda miundombinu, huku akihimiza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira.


Bura ametoa kauli hiyo Septemba 29, 2026, baada ya kutembelea banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayoendelea mkoani Geita.


Amesema wananchi wana nafasi muhimu katika kulinda miundombinu ya umeme kwa kutoa taarifa mapema kuhusu changamoto, ikiwemo nguzo zilizo katika hatari ya kuanguka na miundombinu mingine inayoweza kusababisha madhara.


Amesisitiza pia umuhimu wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati, akisema uelewa huo unaweza kusaidia kuongeza usalama wa miundombinu na kuboresha huduma za umeme.


Bura ameipongeza TANESCO kwa kutumia teknolojia na mifumo ya mawasiliano katika kuboresha huduma kwa wananchi, akisema hatua hiyo imewezesha changamoto kushughulikiwa kwa haraka na kupunguza malalamiko.


Amesema katika baadhi ya maeneo, wananchi wamekuwa wakipata huduma kwa urahisi kupitia vikundi vya mawasiliano vinavyowaunganisha na watendaji wa TANESCO, hivyo kupunguza ulazima wa kufika ofisini kufuatilia changamoto za umeme.


Katika suala la mazingira, Bura amewataka wananchi kupunguza matumizi ya nishati zinazotokana na ukataji wa miti na kutumia nishati safi, akisema matumizi makubwa ya kuni na mkaa yanaweza kuchangia uharibifu wa mazingira.


Amesema Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia fursa zinazotolewa na TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwemo matumizi ya majiko yanayotumia teknolojia za kisasa.


Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Geita, Lucas Swere, amesema TANESCO inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi.


Swere amesema TANESCO imeleta majiko ya kisasa yenye lengo la kurahisisha shughuli za upishi na kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira.


Ametaja baadhi ya majiko hayo kuwa ni yanayotumia mfumo wa pressure cooker pamoja na majiko ya teknolojia ya induction.


Amewahimiza wananchi kutembelea banda la TANESCO katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, utunzaji wa mazingira na teknolojia zinazoweza kurahisisha shughuli za kila siku majumbani.


Kwa mujibu wa viongozi hao, matumizi ya nishati safi yanaweza kusaidia kupunguza ukataji wa miti, kuhifadhi mazingira na kuongeza matumizi ya teknolojia zinazorahisisha shughuli za wananchi.