September 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Jongo akemea chuki za udini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Tabora

WAUMINI wa dini mbalimbali hapa nchini wametakiwa kupendana na kushirikiana katika masuala yote ya kijamii,kiuchumi na kujiepusha na chuki kwa kuwa haileti maendeleo bali inachochea ugomvi na mafarakano.

Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa Sheikh Hamid Jongo kwenye Maulid ya Kumbukumbu ya Mazazi ya Mtume Muhammad S.A.W yaliyofanyika eneo la Stendi ya Zamani Mjini Tabora.

Ameeleza kuwa hakuna dini inayofundisha chuki miongoni mwa waumini wake au kuchukia dini nyingine, hizo ni fikra ovu za watu au mtu binafsi.Hivyo akaonya watu wanaohamasisha chuki au ubaguzi kwa kigezo cha dini.

Sheikh Jongo ameweka wazi kuwa Mtume Muhammad S.A.W alijali utu wa kila mtu wala hakubagua yeyote kwa misingi ya dini na kuongeza kuwa vitabu vitakatifu vya dini zote vinasisitiza upendo na amani.

“Ndugu zangu waislamu, tofauti ya imani sio sababu ya kuchukiana, hata Mwenyezi Mungu hapendezwi na tabia za namna hii, uislamu haufundishi kuchukiana, hizo ni tabia binafsi za mtu, tujiepushe nazo,”ameeleza.

Hata hivyo amesistiza kuwa Mwenyezi Mungu anapendezwa na upendo, amani na mshikamano miongoni mwa jamii na hayo ndiyo yanayochochea maendeleo ya Taifa lolote lile, chuki na mafarakano ni adui mkubwa wa maendeleo.

Amesema,amani iliopo hapa nchini ni kwa sababu ya roho tuliyonayo ya kuvumiliana, kushikamana na kupendana, hivyo akasisitiza waumini kuvumiliana na kila mtu kusali dini anayopenda pasipo kuchukiwa na mwingine.

Akitoa salamu katika hadhara hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Pwani Abas Mtupa amewataka waislamu wote kuendelea kudumisha mshikamano wao na kufanya kazi ili kujiletea maendeleo.

Amepongeza juhudi nzuri na za kimaendeleo zinazoendela kufanywa na Shekhe wa Mkoa wa Tabora Alhaj Ibrahimu Mavumbi na wenzake kwa kuwa zinalenga kuifanya BAKWATA kuwa taasisi yenye uwezo mkubwa kiuchumi.