Na Joyce Kasiki, Geita
KAMPUNI inayojihusisha na uchimbaji wa Madini Chini ya Ardhi Barani Afrika, African Underground Mining Services (AUMS), kwa kushirikiana na kampuni ya Kitanzania, imesema inaendelea kuchangia pato la Taifa kupitia uzalishaji wa madini na kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hiyo.
Akizungumza katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita,mbele ya Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa alipotembele banda hilo mwakilishi wa kampuni hiyo, Saad Simba, amesema AUMS imeweka mkazo katika utekelezaji wa sera ya local content, ikiwemo kutoa ajira na fursa za biashara kwa Watanzania na kampuni za ndani.
Simba alisema takribani asilimia 98 ya manunuzi ya kampuni hiyo yanafanyika ndani ya Tanzania, hatua inayosaidia kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika shughuli za uchimbaji wa madini.
“Kwa upande wa local content tunafanya vizuri. Takribani asilimia 98 ya manunuzi yetu yanafanyika ndani ya nchi, lakini pia tumetoa nafasi kwa kampuni za Kitanzania kujifunza na kushiriki katika shughuli zetu,” amesema Simba.
Aidha, amesema kampuni hiyo imefungua kituo cha mafunzo mjini Geita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuwapatia vijana wa Kitanzania ujuzi wa kuendesha na kutumia mitambo mikubwa inayotumika katika uchimbaji wa madini chini ya ardhi.
Simba amesema kituo hicho kinawapa vijana fursa ya kupata ujuzi wa kitaalamu unaoweza kuwawezesha kushiriki zaidi katika sekta ya madini na kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania.
Amesema AUMS pia inaendelea kushirikiana na Tume ya Madini pamoja na Wizara ya Madini katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
“Tunashirikiana na Tume ya Madini na Wizara ya Madini katika shughuli mbalimbali za kuchangia maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania,” amesema Simba.
Kwa upande mwingine, Simba amesema kampuni mama ya AUMS, Perenti, inaendesha shughuli za uchimbaji katika maeneo mbalimbali nje ya Geita, huku ikiendelea kuangalia namna ya kutumia teknolojia na utaalamu unaopatikana nchini katika kuendeleza sekta ya madini.
Kwa upande wa Tanzania amesema kampuni hiyo inaendelea na mradi wake mmoja, huku ikilenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji, teknolojia na huduma zinazohusiana na sekta ya madini.
Kwa upande wake Dkt.Kirushwa ameipongeza kampuni kwa jitihada ambazo inafanya ikiwemo kuchangia katika pato la Taifa.

More Stories
Watoto waathirika wa moyo, jamii yatakiwa kutambua dalili
Magu yashauriwa kuainisha shule zenye elimu jumuishi
STAMICO, FDH Tanzania zapanua fursa kwa watu wenye ulemavu