Na Joyce Kasiki, Geita

WALIMU wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameonesha ubunifu wa mavazi maalumu ya kujikinga na ajali kwa wafanyakazi wa migodini, katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika maonesho hayo, mwalimu wa ushonaji kutoka VETA Mwanza, Veronica Gabrieli, amesema chuo hicho kinatoa mafunzo yanayozingatia mahitaji ya soko la ajira, ikiwemo utengenezaji wa mavazi ya usalama yanayotumika katika maeneo ya kazi, hususan migodini.
Gabrieli amesema mavazi hayo ni pamoja na overoli, makoti na mavazi mengine maalumu yanayomlinda mfanyakazi wakati wa kutekeleza majukumu yake, huku baadhi yakiwa na rangi zinazoonekana kwa urahisi ili kuongeza usalama katika mazingira ya migodi.
Amesema ushiriki wa VETA katika maonesho hayo pia unalenga kutangaza uwezo wa taasisi hiyo katika mafunzo na uzalishaji, pamoja na kuwaunganisha walimu na wanafunzi na wadau wanaohitaji huduma za utengenezaji wa mavazi mbalimbali kwa ajili ya taasisi na kampuni zao.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Sanaa na Ubunifu pamoja na Teknolojia ya Nguo kutoka VETA Kawa, Eliaichi Lauo, amesema wamewasilisha mavazi mbalimbali yanayolenga kuimarisha usalama na usafi mahali pa kazi, yakiwemo mavazi ya wachimbaji, fulana zenye vimulimuli na makoti yanayotumika na wahudumu wa chakula katika maeneo ya migodi.
Lauo amesema VETA Kawa pia imekuwa ikitengeneza sare kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo sare za walinzi, wanafunzi na wafanyakazi wa viwandani, huku akieleza kuwa chuo hicho kina uwezo wa kuzalisha sare nyingi kwa muda mfupi kutokana na kutumia wataalamu pamoja na kuwashirikisha wanafunzi katika shughuli za uzalishaji.
Ameongeza kuwa fundi mmoja anaweza kushona takribani mavazi 10 hadi 15 kwa siku, hivyo akiwapo kundi la mafundi wengi uzalishaji huongezeka na kuwezesha kukidhi mahitaji ya wateja kwa wakati, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kupata mafunzo katika vyuo vya VETA ili kujengewa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

More Stories
Range ang’ara riadha BAMATA
Wanawake wa Kiislamu waaswa kutumia mitandao kujenga uchumi
NHIF, Aga Khan kuimarisha huduma za saratani Nchini