September 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMDA yaonya kuhusu chanjo bandia ya mifugo sokoni

Na. Mwandishi Wetu,TimesMajira

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Tanzania Veterinary Laboratory Agency (TVLA), imefanikiwa kubaini uwepo wa chanjo bandia aina ya Temevac NDV Strain 1-2 katika soko.

Katika taarifa yake kwa Umma, TMDA imesema uchunguzi umebainisha kuwa chanjo hiyo bandia haikuzalishwa na TVLA na inasambazwa na wafanyabiashara wasiowaaminifu wakitumia lebo zilizogushiwa za chanjo halisi ya Temevac NDV Strain I-2.

Aidha, chanjo hiyo bandia ina mapungufu mbalimbali kama: Kwenye chanjo halisi, nembo ya TVLA ina picha ya darubini (microscope), wakati chanjo bandia ina picha ya kuku. Upande wa kushoto wa lebo ya chanjo halisi una mng’ao wa aluminiamu, wakati chanjo bandia haina.

Lebo ya chanjo halisi ina taarifa zote muhimu ikijumuisha tarehe ya kutengenezwa, tarehe ya kuisha muda wa matumizi, na namba ya toleo, wakati chanjo bandia haina namba ya toleo.

Aidha, wauzaji wote wa dawa za mifugo (wa jumla na rejareja) pamoja na wamiliki wa kliniki za mifugo wameshauriwa kukagua lebo za chanjo hizo kwa umakini mkubwa.

Endapo chanjo hiyo itabainika, inaelekezwa kusitisha matumizi yake mara moja ili kuepusha madhara kwa mifugo, na kutoa taarifa haraka katika ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Songea, Tabora, na Geita, au kupitia simu ya bila malipo 0800110084.