Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imetenga zaidi ya sh. milioni 620 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku vikundi vinavyosuasua kurejesha mikopo vikihimizwa kufanya hivyo haraka ili kutoa fursa kwa wengine kujikwamua kiuchumi.
Hayo yameelezwa Septemba 14,2026 na Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abdullahman Kange, katika kilele cha Mwezi wa Maendeleo ya Jamii kwa halmashauri hiyo kilichofanyika eneo la Kontena, ambapo amewataka Maofisa Maendeleo ya Jamii kuwapongeza na kuwaongezea fedha vikundi vinavyofanya vizuri.Akitolea mfano wa kikundi cha Kilimahewa kilichopata sh.milioni 15 na kurejesha kwa wakati, akisema hatua hiyo inapaswa kuigwa na wengine.

Kange amesema,lengo ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo kutoka hatua moja kwenda nyingine,hivyo alwataka wenye vikundi ambavyo bado havijachukua fedha kujifunza kutoka kwa vilivyokwisha pata mikopo, akisisitiza kuwa fedha hizo zinalenga kusaidia shughuli za kiuchumi, kukidhi mahitaji na kuongeza mitaji ya biashara huku akisitiza kuwa kuchelewesha marejesho kunawanyima wengine fursa ya kujiendeleza.
Pia amesema,dirisha la maombi ya mkopo wa asilimia 10 limefunguliwa na mwisho ni Oktoba 3, 2026,hivyo vikundi vilivyopo Ilemela vinapaswa kuchangamkia fursa hiyo, huku vikundi vinavyosuasua vikionywa kuwa halmashauri itachukua hatua kuhakikisha fedha zinarudi.
Kwa upande wake, Ofisa Usajili wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Yusuph Okoko amesema,maadhimisho hayo ni maelekezo ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu, ambapo kila Septemba huadhimishwa mwezi wa Maendeleo ya Jamii, ambapo shughuli zinazotekelezwa na idara hiyo uoneshwa kwa jamii zikiwemo za vikundi, miradi ya maji na barabara.
Okoko amesema,Maendeleo ya Jamii ni kiungo kati ya Serikali na wananchi, ambapo Maofisa Maendeleo ya Jamii hutambua mahitaji ya wananchi na kusaidia kutafuta namna ya kuyatatua hivyo maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa jamii kufahamu kazi zinazofanywa na idara hiyo.

Mmoja wa wanakikundi cha Furaha Ustawi kutoka Kata ya Buzuruga, Rehema Misana amesema,walianza kupata mkopo mwaka 2018 wa sh. milioni 2 na baadaye kufikia sh.milioni 10, ambao waliweza kuurejesha kwa wakati.
Ambapo amesema,fedha hizo zimewasaidia kukuza shughuli zao kutoka kutengeneza sabuni za maji na mche hadi kuwa na “garment” kubwa ya ushonaji nguo eneo la Buzuruga na kwa sasa wameomba mkopo wa sh.milioni 30 ili kupanua zaidi biashara yao.
Amesema,mikopo hiyo imewasaidia wanakikundi kupata maendeleo, ikiwemo kuacha upangaji, kununua viwanja, kujenga nyumba na kusomesha watoto, pamoja na kuondokana na mikopo ya kausha damu.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Septemba 14, 2026, yaliambatana na kliniki maalum ya maendeleo ya jamii iliyowakutanisha wananchi, makundi yaliyowezeshwa na Halmashauri na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo na kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050, chini ya kaulimbiu “Familia Imara, Uchumi Imara, Taifa Imara”.


More Stories
NMB yaingia 10 Bora Duniani
Yas yaboresha mazingira ya elimu Buigiri, Dodoma
Waziri Salome ashiriki ufunguzi Gastech 2026 Bangkok