September 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yatakiwa kuimarisha utabiri wa hali ya hewa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Abdallah Mitawi, ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, utabiri na utoaji wa tahadhari za mapema akisema TMA ni taasisi kiungo katika maendeleo ya sekta zote nchini, zikiwemo kilimo, miundombinu, biashara na huduma mbalimbali.

Mitawi amesema nchi inahitaji kuwa na taasisi imara ya hali ya hewa yenye wataalamu, teknolojia na vifaa vinavyoendana na wakati akisisitiza kuwa taarifa za utabiri zinapaswa kuzingatiwa tangu hatua za awali za utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo akionya kupuuzia taarifa hizo kunaweza kuhatarisha uwekezaji na kufanya maendeleo yasidumu.

Ameipongeza TMA kwa kutambuliwa kuwa Center of Excellence katika Afrika Mashariki na ngazi ya kikanda na kusema mafanikio hayo yanaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inayolenga Tanzania kuwa kinara wa maarifa na ubunifu ambao nchi nyingine za Afrika na dunia zinaweza kujifunza.

Aidha, Mitawi ameipongeza TMA kwa kufikia usahihi wa utabiri wa hali ya hewa wa asilimia 89.1 akisema mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika teknolojia, ametaja pia matumizi ya Akili Bandia (Al) katika kuimarisha utabiri na kuitaka TMA kuendelea kuboresha teknolojia hizo ili kuwa miongoni mwa taasisi bora duniani.

Kuhusu taarifa za mvua zinazohusishwa na El Nino, ameipongeza TMA kwa kuendelea kutoa taarifa kwa umma na taasisi zinazoweza kuathirika na kuitaka kuongeza ushirikishwaji wa wadau wakiwemo TAMISEMI, Wizara ya Elimu, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama hatua itakayosaidia maandalizi na mwitikio wa mapema.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema Mamlaka inaendelea kufuatilia hali ya hewa, kutoa utabiri na tahadhari za mapema na kusisitiza kuwa TMA itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali na kutoa elimu kwa umma.

Akitoa wasilisho kuhusu shughuli za TMA, Egidius Bonyeza amesema Mamlaka inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, uchambuzi na utabiri na kuongeza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa yataendelea kupewa kipaumbele.