September 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Haule aungana na wananchi kuchimba msingi wa shule

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Diwani wa Kata ya Utengule, Haule, ameungana na wananchi wa eneo hilo kuchimba msingi wa ujenzi wa shule, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Haule alishiriki kazi hiyo pamoja na wananchi, hatua iliyolenga kuhamasisha jamii kuendelea kujitolea katika ujenzi wa miundombinu ya elimu na miradi mingine yenye manufaa kwa wananchi.

Nguvu na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kushiriki ujenzi wa shule hiyo, umemvutia Haule ambaye amewapongeza kwa kujitolea kwao, akisema ushiriki huo ni chachu ya maendeleo ya jamii.

Wananchi hao wamejitokeza kwa wingi kushiriki kazi hiyo kwa kujitolea, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyotenga Sh583 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo unatarajiwa kuondoa adha kwa wanafunzi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya elimu ya sekondari katika maeneo mengine.

Akizungumza baada ya kushiriki zoezi hilo, Haule amesema ameguswa na moyo wa kujitolea ulioonyeshwa na wananchi, wakiwemo vijana, wanawake na wazee.

Amesema ujenzi wa shule hiyo umekuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi, hali iliyowasukuma kujitokeza kwa wingi kushiriki kazi za ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

“Nilipofika hapa na kuona wananchi wa makundi mbalimbali wakijitolea kwa nguvu zao kuchimba msingi wa shule hii, niliona ni muhimu nami kushiriki nao. Hii inaonesha namna wananchi walivyokuwa na kiu ya kupata shule katika eneo lao,” amesema Haule.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbalizi, Paul Mwampamba, amesema zoezi hilo limekuwa shirikishi, huku wananchi wakionesha mshikamano mkubwa kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa watoto wao.

Amesema kwa muda mrefu wanafunzi wa eneo hilo wamekuwa wakilazimika kusoma katika shule za mbali, zikiwemo Shule za Sekondari Juhudi na Usongwe, hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu kila siku.

Kwa mujibu wa Mwampamba, uwepo wa shule hiyo karibu na makazi ya wananchi utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wanapokuwa njiani kwenda na kurudi shuleni.

Naye Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya Usongwe, Fatma Issa, amesema ushiriki mkubwa wa wananchi katika zoezi hilo ni ishara ya mshikamano na utayari wao wa kushirikiana na viongozi katika kuleta maendeleo.

Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kushiriki katika hatua nyingine za utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa watoto wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa shule hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 41,904 wa maeneo yanayozunguka Shigamba Pipeline, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa wananchi wa eneo hilo.