
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imesema imejipanga kuhakikisha mradi wa uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Mto Songwe unaendelea kutunzwa na kuendelezwa kwa manufaa ya jamii inayozunguka bonde hilo.
Aidha, wataalamu kutoka sekta mbalimbali wameelekezwa kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara na kuwasilisha taarifa kila baada ya robo mwaka ili kuhakikisha shughuli na mafanikio ya mradi huo yanaendelezwa kikamilifu.
Kauli hiyo ilitolewa Septemba 3, 2026, na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, Aida Haule, wakati wa hafla ya kupokea mradi wa uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Mto Songwe.
Mradi huo umetekelezwa chini ya ushirikiano wa Tume ya Pamoja ya Tanzania na Malawi inayoshughulikia uhifadhi na uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe, ambalo maji yake hatimaye humwaga katika Ziwa Nyasa.

Akisoma taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mbele ya ugeni kutoka Wizara ya Maji, Afisa Kilimo wa halmashauri hiyo, Aidan Mlawa, amesema mradi huo ulitekelezwa katika Tarafa ya Isangati, hususan katika kata za Izyra na Iwiji.
Amesema utekelezaji wa mradi ulihusisha vijiji vinne vya Izyra, Isende, Masewe na Izumbwe II.
Kwa mujibu wa Mlawa, mradi huo ulilenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi wanaoishi na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vyanzo na kingo za mito inayomwaga maji katika Mto Songwe.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwapatia wananchi shughuli mbadala za kiuchumi ili kupunguza utegemezi wa shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji na kandokando ya mito.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji, Sehemu ya Maji Shirikishi kutoka Wizara ya Maji, Florence Mahay, amesema mradi huo umefanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali mbadala za kiuchumi, ikiwemo ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Amesema jumla ya ng’ombe 40 wa maziwa wamegawiwa kwa vikundi tisa vya wafugaji katika vijiji vya Masewe, Izyra, Isende na Izumbwe II.
Naye Mratibu wa Miradi ya Bonde la Mto Songwe kutoka Wizara ya Maji, Mwanamkuu Mwanyika, amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza kwa kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta mbalimbali zinazohusika.
Sekta hizo ni pamoja na mazingira, kilimo, mifugo, uvuvi na samaki, misitu pamoja na maendeleo ya jamiiAmesema ushirikishwaji wa wataalamu kutoka sekta mbalimbali umekuwa muhimu katika kuhakikisha uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Mto Songwe unatekelezwa kwa mtazamo jumuishi na kuleta manufaa endelevu kwa jamii.

More Stories
TMA yatakiwa kuimarisha utabiri wa hali ya hewa
Haule aungana na wananchi kuchimba msingi wa shule
WMA yatahadhari wanaochezea mizani