Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano Yas Tanzania, imetambulisha rasmi uzi/jezi mpya zitakazovaliwa na washiriki wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku maandalizi yakishika kasi kuelekea msimu wa sita wa mbio hizo zinazotarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 10,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Uzi huo mpya ulitambulishwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua nyingine muhimu kuelekea kwenye kilele cha mbio hizo zitakazofanyika visiwani Zanzibar Septemba 20 mwaka huu.
Mbio za Yas Zanzibar International Marathon zimeendelea kukua na kuwa zaidi ya mashindano ya riadha, zikitoa fursa ya kuhamasisha maisha yenye afya, kukuza utalii wa michezo na kuitangaza Zanzibar kama moja ya vivutio vya utalii.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa jezi hizo, Meneja Chapa na Mawasiliano wa Yas Tanzania, Woinde Shisael, amesema, Marathon hiyo inawapa washiriki nafasi ya kukimbia huku wakifurahia upekee wa Zanzibar.
“Wakimbiaji wanapovaa jezi hii, tunataka wajisikie kuwa sehemu ya tukio la kipekee. Hawaji Zanzibar kwa ajili ya kukimbia pekee, bali pia kuifurahia utalii wa Zanzibar, kukutana na watu kutoka maeneo mbalimbali na kuwa sehemu ya tukio linalounganisha michezo, afya na utalii,” amesema Shisael

Kwa upande wake mmoja wa waratibu wa mbio hizo za Yas Zanzibar International Marathon, Salim Kikeke alisema maandalizi yanaendelea vizuri huku wakijiandaa kuwapokea wakimbiaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Utambulisho wa jezi hizi unatupeleka hatua nyingine ya kuhakikisha kila mshiriki anapata uzoefu wa kipekee kuanzia anapojisajili hadi anapovuka mstari wa mwisho. Tunawahamasisha wale ambao bado hawajajisajili kufanya hivyo mapema,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Masoko – Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahma Sanya amehamasisha watanzania kujitokeza kwa wingi akieleza namna mbio hizo zinavyosaidia kuchochea utalii wa michezo Zanzibar, huku ujio wa wakimbiaji na wageni ukifungua fursa kwa mahoteli, migahawa, huduma za usafiri na biashara nyingine zinazohudumia sekta ya utalii.
Mbio za mwaka huu zimebeba kaulimbiu ya “Kasi Swadakta kwa Viwango.” ikimaanisha kuwa mwaka huu washiriki wote watapata uzoefu (experience) yenye viwango vya kimataifa huku wakifurahia mtandao swadakta wa viwango wa Yas.
Washiriki wanaweza kujisajili na kufanya malipo kidijitali kupitia Mixx kwa kupiga 15001#, kuchagua 5 (Lipa kwa Simu), 6 (Tiketi), 1 (Marathon) na kisha kuchagua Zanzibar Marathon na kukamilisha malipo.
Yas Zanzibar International Marathon 2026 itakuwa na mbio za kilomita 5, kilomita 10 na kilomita 21, zitakazowakutanisha wanariadha wa kulipwa, wakimbiaji wa kawaida, familia na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.

More Stories
Ilemela yatakiwa kusimamia mifumo ukusanyaji mapato
Msigwa:Usikubali kumsajilia mtu laini ya simu
Fahari ya Z’bar 2026 kuwakutanisha wazalishaji zaidi ya 300