September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Salome:Wizara ya Nishati inajukumu kutoa umeme wa uhakika

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

NAIBU Waziri wa Nishati,Salome Makamba, amesema jukumu kuu la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wanapatiwa taarifa kwa wakati pindi changamoto zinapojitokeza.

Makamba ameyasema hayo leo, tarehe 01 Septemba 2026, wakati akijibu Swali la Exaud Silaoneka Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, aliyetaka kufahamu lini Serikali itabadilisha mkataba wa usambazaji wa umeme kwa wananchi kutoka Mwenga Power kwenda TANESCO, ili Mwenga Power ibaki kuwa mzalishaji wa umeme.

Akijibu swali hilo, Makamba amesema utoaji na usimamizi wa leseni za uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini ni jukumu la kisheria la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kwa mujibu wa Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na taratibu za utoaji wa leseni hizo.

“Jukumu namba moja la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wanapata taarifa kwa wakati kunapotokea changamoto,” amesema Makamba.

Ameeleza kuwa uamuzi wowote wa kubadili muundo wa leseni ya usambazaji umeme katika eneo hilo unapaswa kuzingatia matakwa ya sheria na taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo, Makamba amesema Serikali, kwa kutambua kuwa kumekuwa na malalamiko kuhusu ubora wa huduma inayotolewa na Mwenga Power, tayari taasisi zake za EWURA, TANESCO na REA zimeanza kufanya tathmini ya kina ili kubaini uwezekano wa kufanya mabadiliko hayo bila kuathiri uwekezaji uliopo.

Amesema tathmini hiyo itafanyika kwa haraka ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme yenye uhakika na inayokidhi mahitaji yao.

Aidha, akihitimisha, Makamba amesema yupo tayari, pindi Vikao vya Bunge vitakapokamilika, kuongozana na Exaud Silaoneka Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kwenda kusikiliza na kufahamu kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi katika eneo hilo.