
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
TAASISI ya Tulia Trust imeanza kumjengea nyumba Bibi Grace Deya (70), mkazi wa Tembela, Jimbo la Uyole, aliyekuwa akiishi katika nyumba chakavu huku akiwalea watoto wake watatu wenye changamoto za afya ya akili.
Hatua hiyo inalenga kumwondolea kikongwe huyo mzigo wa maisha ya kutegemea msaada wa majirani kupata chakula, mavazi, malazi na mahitaji mengine muhimu kwa ajili yake na watoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari , Agosti 27, Ofisa Uhusiano na Mahusiano wa Tulia Trust, Joshua Mwakanolo, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya uongozi wa Mtaa na Kata ya Tembela kufanya tathmini na kubaini ukubwa wa changamoto zinazoikabili familia hiyo.

Amesema ujenzi huo ni sehemu ya shughuli za Tulia Trust katika kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, huku nyumba hiyo ikitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa Bibi Deya Septemba 25, mwaka huu.
“Tumeangalia changamoto alizonazo huyu bibi na kubaini kuwa ni kubwa zaidi kuliko familia nyingine. Tunaamini nyumba hii itajengwa kwa haraka zaidi na tutaikabidhi Septemba 25,” amesema Mwakanolo.
Mwakanolo amesema hadi sasa Tulia Trust imejenga nyumba 26 katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya, zikiwamo mbili mkoani Morogoro na nyingine mkoani Ruvuma.
Akizungumza kupitia mkalimani, Bibi Deya amesema maisha yake yamekuwa magumu tangu mumewe alipofariki miaka 10 iliyopita, huku akilazimika kuomba msaada ili aweze kuishi na watoto wake.
“Nawashukuru sana ndugu zangu na hasa Tulia kwa kuniona mimi, kwa sababu maisha yangu yalikuwa magumu. Nilikuwa naishi kwa kuomba. Mume wangu alifariki miaka 10 iliyopita na watoto wangu wana changamoto za afya ya akili,” amesema.

Ndugu yake, Kimaro Mwayonga, amesema watoto hao wakati mwingine wamekuwa wakimtesa mama yao, akieleza kuwa hali hiyo imeongeza ugumu wa maisha kwa Bibi Deya ambaye amekuwa akitegemea majirani.Diwani wa Kata ya Tembela, Frank Mwasyoke, amesema mbali na ujenzi wa nyumba hiyo, Dkt. Tulia amekuwa akisaidia wananchi katika huduma za afya, ambapo zaidi ya watu 300 wamewezeshwa kupata bima, akisema msaada huo umeleta tabasamu kwa wananchi wa kata hiyo.

More Stories
Ushirikiano NHIF na ZHSF wavutia Kamati ya Bajeti
EAC yahimiza ushirikiano wa Kikanda katika elimu
Yas yamwezesha mtangazaji kuripoti matukio Mlima Kilimanjaro