Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KAMATI ya Bajeti ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa juhudi zake za kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za bima ya afya nchini, pamoja na ushirikiano wake na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF).
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 26, 2026, na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Hamis Said, wakati Kamati hiyo, ikishirikiana na Menejimenti za ZHSF na NHIF, ilipotembelea Makao Makuu ya NHIF kwa ajili ya kujifunza namna Mfuko huo unavyoendesha shughuli zake na kutoa huduma kwa wanachama.
Mariam amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa, kwa kuwa Kamati imepata fursa ya kuelezwa na kujionea kwa vitendo mifumo na huduma zinazotolewa na NHIF, ikiwemo kupitia ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).
Pamoja na kuipongeza NHIF, Kamati hiyo ilipata fursa ya kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji na maendeleo ya Mfuko huo, ikiwemo namna NHIF inavyokabiliana na udanganyifu, utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora na kwa wakati.
Aidha, Kamati ilitaka kufahamu namna matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) yalivyoboresha utendaji wa NHIF na kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji, pamoja na mchango wa uwekezaji katika kuimarisha Mfuko.
Masuala mengine yaliyopewa uzito ni vyanzo vya mapato ya Mfuko, viashiria vinavyotumika kupima mafanikio na uendelevu wa NHIF, pamoja na mafunzo na uzoefu ambao Mfuko umeupata katika kipindi cha miaka 25 ya utekelezaji wa majukumu yake.
Mariam amesema ushirikiano kati ya NHIF na ZHSF umeleta matokeo makubwa katika hatua mbalimbali za uanzishaji na uendelezaji wa ZHSF, huku akieleza kuwa uzoefu na msaada uliotolewa na NHIF umeiwezesha Zanzibar kuanza na kuendelea vizuri katika safari ya kuimarisha huduma za bima ya afya.
“Kamati inapongeza NHIF na ZHSF kwa mashirikiano makubwa wanayoyafanya ambayo yamewezesha ZHSF kuanza na kuendelea vizuri,” amesema.
Ameongeza kuwa kazi iliyofanywa na NHIF katika kusaidia uanzishaji wa ZHSF ilihitaji uvumilivu na kujitolea kwa kiwango kikubwa, akieleza kuwa Zanzibar imenufaika na uzoefu wa NHIF katika kujenga mfumo wa bima ya afya.
“Kazi iliyofanywa na NHIF ni kazi iliyofanyika kwa uvumilivu mkubwa, lakini kwa kutubeba Zanzibar katika uanzishaji wa Mfuko wetu,” amesema.
Aidha, Mariam ameipongeza Menejimenti ya NHIF kwa kuwawezesha kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambako wamejionea namna wanachama wa NHIF wanavyopokelewa na kuhudumiwa.
Amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kuona kwa vitendo ubora wa huduma zinazotolewa, hususan huduma za kibingwa na kibingwa bobezi, akieleza kuwa hali hiyo ni miongoni mwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya nchini.
“Tumejionea namna wanachama wa NHIF wanavyopokelewa na kuhudumiwa. Hakika kazi hii ni kubwa na nzuri ambayo kwa ujumla tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo huduma za kibingwa na kibingwa bobezi zinapatikana hapa nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema Mfuko utaendelea kushirikiana kwa karibu na ZHSF kuhakikisha wananchi na wanachama wanapata huduma bora za afya kwa wakati na kwa ufanisi.
Dkt. Isaka amesema NHIF itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa ZHSF, hususan katika maeneo ya uzoefu, mifumo ya utoaji huduma na masuala mengine ya kitaalamu, kwa lengo la kuimarisha huduma za bima ya afya kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya NHIF kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wananchi popote walipo nchini, huku mifuko hiyo ikiendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha huduma kwa wanachama.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma za bima ya afya Tanzania Bara na Zanzibar.

More Stories
Tulia amfuta machozi Bibi mlezi Watoto wenye afya ya akili
EAC yahimiza ushirikiano wa Kikanda katika elimu
Yas yamwezesha mtangazaji kuripoti matukio Mlima Kilimanjaro