Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WANAFUNZI na vijana nchini wamepata fursa mpya ya kujifunza, kufanya majaribio na kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia baada ya Airtel Africa Foundation kuzindua upya jengo la Airtel Fursa Lab katika Shule ya Sekondari Kijitonyama, Dar es Salaam, lililofanyiwa ukarabati.
Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2020 kwa ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), kimekuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha wanafunzi, walimu na vijana kupata ujuzi wa kidijitali, biashara na ubunifu.
Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya watu 5,800, wakiwemo wanafunzi, walimu, vijana, wajasiriamali na wanawake, wamenufaika na programu mbalimbali zinazotolewa kupitia Fursa Lab.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo lililokarabatiwa jana, Mkuu wa Programu kutoka Airtel Africa Foundation,Esi Prah, amesema uwekezaji huo unalenga kuwapatia vijana mazingira bora na zana zinazowawezesha kujifunza na kutumia teknolojia kwa vitendo.
“Tunaamini kuwa upatikanaji wa teknolojia na elimu ya kidijitali unaweza kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapatia maarifa, ujasiri na ujuzi wanaohitaji ili kutengeneza suluhisho mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,”amesema Prah.
Amesema Fursa Lab imejengwa katika dhana ya kuwapa vijana nafasi ya kujifunza, kujaribu mawazo yao na kutumia teknolojia kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
Kituo hicho kinawawezesha vijana kujifunza maeneo mbalimbali, yakiwemo sayansi ya kompyuta, programu za kompyuta, biashara, stadi za maisha, chakula na lishe, pamoja na ushonaji na ubunifu.
Aidha, Fursa Lab imewaunganisha wanafunzi na majukwaa mbalimbali ya kujifunzia, yakiwemo ShuleDirect, Maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na WazoLearn, pamoja na maudhui yanayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI).
Kwa miaka kadhaa, kituo hicho kimekuwa pia sehemu ya kukuza vipaji na ubunifu kwa wanafunzi, huku baadhi yao wakipata nafasi ya kushiriki katika programu mbalimbali na kuwa mabalozi wa UNICEF na Plan International, wabunifu wa Oky, wasanii wa kidijitali pamoja na wabunifu katika maeneo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
Miongoni mwa ubunifu uliofanywa na wanafunzi ni programu ya kufuatilia mzunguko wa hedhi iliyolenga kuwasaidia wasichana kupata taarifa na kufuatilia mizunguko yao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, amesema ukarabati na ufunguzi upya wa Fursa Lab unaakisi dhamira ya kampuni ya kupanua fursa za elimu ya kidijitali kwa vijana nchini.
“Ukarabati na ufunguzi upya wa Airtel Fursa Lab unaakisi dhamira yetu ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata zana, maarifa na fursa wanazohitaji ili kufanikiwa katika dunia ya kidijitali,” amesema Singano.
Amesema Airtel inalenga kuhakikisha teknolojia inatumika kama nyenzo ya elimu, ubunifu na kujenga fursa za kiuchumi, badala ya kubaki kuwa chombo cha mawasiliano pekee.
Singano amesema kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, Airtel imeunga mkono zaidi ya shule tano na itaendelea kufanya kazi na washirika wake kuwafikia vijana na jamii nyingi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kijitonyama, Halima Juma, amesema Airtel Fursa Lab imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya shule hiyo, hasa katika kukuza matumizi ya TEHAMA na ubunifu miongoni mwa wanafunzi.
Uwekezaji huo unaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za elimu katika kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa, ambayo inazidi kutegemea teknolojia na ujuzi wa kidijitali.
Kwa kurejeshwa kwa Fursa Lab katika mazingira mapya, wanafunzi na vijana wanatarajiwa kupata nafasi zaidi za kujifunza kwa vitendo, kubuni teknolojia na kugeuza mawazo yao kuwa suluhisho zinazoweza kusaidia jamii.
Hatua hiyo pia inaweka mkazo katika umuhimu wa kuwajengea vijana uwezo mapema ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kutumia teknolojia kama nyenzo ya kujiajiri, kuanzisha biashara na kutengeneza suluhisho za changamoto zinazozikabili jamii.

More Stories
Kikundi cha Mshikemshike cha badilisha maisha kwa Ufugaji wa Kondoo Shinyanga
NMB yaibuka Superbrand Afrika Mashariki 2026-2028
MNH Mloganzila yaanza kambi ya Upasuaji wa Nyonga,Magoti na Mabega