Na Mwandishi wetu,Timesmajira
KIKUNDI cha Mshikemshike cha Kijiji cha Kimandaguli, Kata ya Lyabukande, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kimeonyesha mafanikio makubwa katika ufugaji wa kondoo baada ya kuongeza idadi ya mifugo kutoka 30 hadi 132 ndani ya kipindi kifupi.
Kikundi hicho kilianza rasmi mwaka 2024 kikiwa na wanachama watano walioungana kwa lengo la kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za ufugaji.

Mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mkopo wa Sh milioni 15 walioupata kutoka serikalini, ambao uliwawezesha kuboresha miundombinu na kupanua shughuli zao za ufugaji.

Tangu walipopata mkopo huo, kikundi kimefanikiwa kuuza kondoo 100 na kupata mapato yaliyowawezesha kuendeleza na kupanua zaidi mradi wao.
Aidha, kikundi hicho kilionyesha nidhamu katika matumizi ya fedha na ulipaji wa mkopo, ambapo hadi sasa tayari kimeweza kurejesha Sh milioni 3.75.
Akizungumza na Timesmajira kwa njia ya simu, Meles Kidebeli, Mmoja wa wadau wanaohusika na utoaji wa mikopo ya Halmashauri kwa vijana katika Halmashauri ya Shinyanga,amesema mikopo hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa vijana na vikundi mbalimbali.

Amesema moja ya faida kubwa ni kwamba mikopo hiyo haina riba, huku wanufaika wakipewa muda wa kutosha wa kurejesha fedha na mchakato wa kuipata ukiwa si mrefu.
“Faida yake kwanza hii mikopo haina riba. Ukipewa milioni 10 unarudisha milioni 10, lakini pia utapewa muda wa kutosha kabla ya kurudisha. Ni mikopo ambayo haina mchakato mwingi kuipata,”Amesema Kidebeli.

Amesema mafanikio ya Kikundi cha Mshikemshike yanaonyesha namna mikopo ya serikali inavyoweza kuwa chachu ya kuongeza uzalishaji, ajira na kipato kwa vijana na wananchi wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi vijijini.
Kwa ongezeko la mifugo kutoka kondoo 30 hadi 132 pamoja na mauzo ya kondoo 100, kikundi hicho sasa kinaendelea kujenga msingi imara wa kukuza biashara yake ya ufugaji na kuongeza kipato cha wanachama wake.

More Stories
AIRTEL FURSA LAB yarudi kwa sura mpya
NMB yaibuka Superbrand Afrika Mashariki 2026-2028
MNH Mloganzila yaanza kambi ya Upasuaji wa Nyonga,Magoti na Mabega