Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeanza rasmi kambi maalum ya upasuaji wa nyonga, magoti na mabega inayofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 29 Agosti 2026, kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya upasuaji wa matundu madogo.
Kambi hiyo inawalenga wagonjwa wenye changamoto za nyonga, magoti na mabega wanaohitaji uchunguzi na matibabu ya kibingwa, ambapo jumla ya wagonjwa 15 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kipindi cha kambi hiyo.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Mifupa na Ajali kutoka MNH-Mloganzila, Dkt. Joseph Jinasa, amesema wataalamu wa hospitali hiyo wanashirikiana na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Goti, Bega, Arthroscopy na Majeraha ya Michezo kutoka nchini India, Dkt. Vinay Tantuway, katika kutoa huduma hizo.

Amesema matumizi ya teknolojia ya upasuaji wa matundu madogo yanawezesha wagonjwa kupata matibabu yenye majeraha madogo, maumivu machache baada ya upasuaji na kupona kwa haraka, hivyo kuwawezesha kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa muda mfupi.
Dkt. Jinasa amesema kambi hiyo pia inalenga kuwajengea wataalamu wa MNH-Mloganzila ujuzi na uzoefu zaidi katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, hususan matumizi ya mbinu za kisasa za upasuaji wa matundu madogo.
Ameongeza kuwa sambamba na upasuaji wa matundu madogo, hospitali itaendelea kutoa huduma nyingine za kibingwa ikiwemo upasuaji wa kubadilisha magoti kwa kutumia magoti bandia, kubadilisha nyonga kwa nyonga bandia pamoja na upasuaji wa marejeo kwa wagonjwa wanaohitaji kurekebishiwa upasuaji wa awali.

Amewahimiza wananchi wenye changamoto za nyonga, magoti na mabega kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa ajili ya uchunguzi na kupata matibabu stahiki kupitia huduma hizo za kibingwa.

More Stories
Viongozi wataka Vijana waongeze ushiriki katika Ubunifu wa Kidijitali Afrika
Serikali yajidhatiti uwezeshaji wanawake kiuchumi
OUT Yaweka Ubunifu Msingi wa Elimu Huria Mtandaoni