Na Catherine Sungura, TimesMajira Online,Dodoma
WATANZANIA wamekumbushwa kuzingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Prof. Abel Makubi Mganga Mkuu wa Serikali , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Wizara jijini Dodoma.
“Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa kama ya kuhara ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema” amsema Prof. Makubi
Prof. Makubi amesema kufuatia kujitokeza kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka hali hiyo ina hatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.
Aidha, Mganga mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuzingatia kanuniz za afya kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa au kutatibu kwa dawa maalumu na kuhakikisha maji ya kunywa nay ale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi
“Tunawapongeza wananchi na ninyi wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwa sababu wananchi wamekuwa wasikivu na kutii masharti ya usafi na jinsi ya kujikinga,ni zaidi ya mwaka na nusu sasa Tanzania tumeweza kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini”.
Aidha, amesema jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama na ushirikiano mzuri wa wananchi na hivyo kusababisha baadhi ya magonjwa yanayotokana na uchafu yamepungua.
Hata hivyo Prof. Makubi amesisitiza kutumia ipasavyo vyoo na hasa kipindi hiki cha mvua kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa,kabla ya kula kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.
“Tuongeze usimamizi wa usafi wa nyumba na hasa usafi wa mikono wananchi wamekua wakihamasika usafi wa mikono katika vipindi mbalimbali,hivyo tungeomba kasi ya kunawa mikono iwe endelevu katika mikusanyiko, mashule, madukani, hospitalini,vituo vya mabasi,na taasisi pamoja na masoko, sehemu za kunawia mikono iwe ndelevu kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafi wa kunawa mikono wa hali ya juu
Pia,amewata waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaelekezwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikaili za mitaa, Wananchi na wadau mbali mbali ili kuhakisha kila eneo lilio chini yao, haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko kwa kutotapisha vyoo au vyovyote vinavyotoka kwenye vyoo kwenda kwenye mazingira ya wananchi.
Kwa upande wa kujikinga dhidi ya kuumwa na Mbu Prof. Makubi amewataka wananchi kutumia ipasavyo vyandarua kabla ya kwenda kulala au wenye uwezo wa kununua dawa za kujipaka wapake ili ziwasaidie.
Prof. Makubi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini na shime kuimarisha afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na tabia za usafi katika familia na jamii kwa ujumla ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi