August 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Teknolojia yarahisisha uendeshaji wa biashara ndogo



Na Joyce Kasiki, Tanga


WAFANYABIASHARA wadogo na wa kati sasa wanaweza kutumia teknolojia kurahisisha usimamizi wa shughuli zao za kila siku kupitia mfumo wa kidijitali unaowawezesha kuhifadhi taarifa na kufuatilia mwenendo wa biashara kwa wakati.


Mfumo huo unatoa nafasi kwa mfanyabiashara kuingiza taarifa za mauzo na shughuli nyingine za biashara, kisha kuzitumia kupata picha ya mwenendo wa biashara kwa vipindi tofauti.


Kwa kutumia taarifa hizo, mfanyabiashara anaweza kutambua namna biashara yake inavyokwenda, kufuatilia mabadiliko ya mauzo na kufanya maamuzi akitumia takwimu badala ya kutegemea makadirio.


Akizungumza katika banda la Chuo Kikuu cha Dodoma kwenye maadhimisho ya wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea jijini Tanga kwenye viwanja vya shule ya sekondari Usagara mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo hiyo anayesoma Shahada ya Biashara katika Mifumo ya Taarifa , Lamway Mogen aliyebuni mfumo wa Kogpos.co.tz amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kupunguza changamoto ya wafanyabiashara kutokuwa na kumbukumbu zilizopangiliwa kuhusu shughuli zao.


Amesema mfumo huo pia unaweza kuwa nyenzo muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, kwa kuwa taarifa za biashara zinapokuwa zimehifadhiwa vizuri zinaweza kutoa ushahidi wa mwenendo wa shughuli za mfanyabiashara.


“Tunataka mfanyabiashara aweze kupata taarifa za biashara yake kwa urahisi na kuzitumia katika kupanga hatua zinazofuata,” amesema.


Aidha, amesema kumbukumbu za miamala na mwenendo wa biashara zinaweza kuchangia katika ujenzi wa credit score, jambo ambalo linaweza kuongeza fursa za mfanyabiashara kutambulika wakati anapotafuta huduma za kifedha.


Kwa mujibu wa mbunifu huyo, matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko katika uendeshaji wa biashara, hasa kwa wafanyabiashara wanaotaka kuongeza ufanisi na kuwa na udhibiti mzuri wa shughuli zao.


Amesema wafanyabiashara wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia ili kuboresha utunzaji wa kumbukumbu, kufuatilia utendaji wa biashara na kupanga mikakati ya kukuza shughuli zao.