August 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubunifu wafungua Njia mpya kufuatilia simu zilizoibwa


Na Joyce Kasiki, Tanga


WATUMIAJI wa simu sasa wanaweza kupata msaada wa teknolojia katika kukabiliana na changamoto ya kupoteza au kuibiwa kwa vifaa vyao, baada ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuja na mfumo unaolenga kurahisisha ufuatiliaji wa simu.


Mfumo huo unaojulikana kama VexGuard Anti-Theft System umebuniwa na Emmanuel Mpyambala, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesoma Uhandisi wa Kompyuta chuoni hapo.


Akizungumza katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Mpyambala alisema mfumo huo unampa mwenye simu nafasi ya kupata taarifa kuhusu kifaa chake hata akiwa anatumia simu nyingine.


Amesema endapo simu imepotea, mhusika anaweza kukopa kifaa cha ndugu au rafiki, kisha akapakua programu husika kupitia Play Store na kuingia kwa kutumia akaunti iliyokuwa ikitumika kwenye simu iliyopotea.


Baada ya kuingia, mfumo huonyesha vifaa vilivyowahi kuunganishwa na akaunti hiyo. Mtumiaji anaweza kuchagua simu inayotafutwa na kupata taarifa ya eneo lake kwa kutumia teknolojia ya GPS.


Mbali na kuonyesha mahali simu ilipo, amesema teknolojia hiyo inaweza kumwezesha mmiliki kuchukua hatua za haraka za kuilinda, ikiwamo kuifunga kwa mbali ili kuzuia matumizi yasiyoruhusiwa.


Mpyambala amesema pia kuna mifumo inayotoa fursa ya kuweka ujumbe au mawasiliano ya mwenye simu kwenye kifaa kilichopotea. Kwa njia hiyo, mtu anayekikuta anaweza kupata namna ya kumtafuta mmiliki.


Hata hivyo, ameonya kuwa ufuatiliaji wa kiteknolojia haupaswi kuchukuliwa kama mbadala wa vyombo vya usalama. Kwa simu ambayo imeibwa, mmiliki anapaswa kuripoti tukio Polisi ili hatua zaidi zichukuliwe.


Amesema taarifa zinazopatikana kuhusu eneo la simu zinaweza kusaidia katika mchakato wa uchunguzi, huku mamlaka husika zikifuata taratibu za kisheria na kutumia njia zinazotambulika kufuatilia kifaa.


Kwa mtazamo wake, kuendelea kuunganisha ubunifu wa kiteknolojia na ushirikiano wa wananchi na vyombo vya dola kunaweza kuwa sehemu ya suluhisho la tatizo la wizi wa simu, pamoja na kuongeza nafasi ya vifaa vilivyopotea kurejea kwa wenyewe.