Na Joyce Kasiki, Tanga
VIJANA walionufaika na mafunzo ya ujuzi kupitia mradi wa Wezesha Binti, unaotekelezwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Enabel Tanzania mkoani Kigoma, wameanza kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuingia katika soko la ajira.
Mradi huo umelenga kuwapatia vijana maarifa na ujuzi unaowawezesha kutumia taaluma walizosomea kujipatia kipato, badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la Enabel katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika jijini Tanga, Afisa Mradi wa Wezesha Binti mkoani Kigoma kutoka Enabel Tanzania, Abel Mbilinyi, amesema vijana 2,350 wamenufaika na mafunzo hayo.
Amesema kati yao, vijana 430 wamefanikiwa kupata ajira baada ya kupata mafunzo ya ujuzi yaliyolenga kuwawezesha kuingia katika soko la ajira na kujiajiri.
“Lengo ni kuendelea kuondoa dhana kwamba maarifa na ujuzi ni kwa ajili ya wale waliofeli. Hapana, bali ujuzi ni kwa ajili ya kila mtu,” amesema Mbilinyi.
Amesema mafunzo hayo yamekuwa muhimu kwa vijana kwa kuwa yanawapa uwezo wa kufanya kazi na pia kutumia ujuzi wao kuanzisha shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato.
Ushiriki wa Enabel katika maadhimisho hayo hauishii kwenye kuonesha kazi na shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo, bali pia umejikita katika kusaidia shughuli zinazolenga kukuza ujuzi wa vijana.
Miongoni mwa maeneo ambayo Enabel imeelekeza nguvu ni Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi ya WorldSkills, yanayofanyika sambamba na Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu jijini Tanga.
Mashindano hayo yanaweka vijana katika mazingira ya kuonesha uwezo wao wa kufanya kazi kwa vitendo na yanatumika kama maandalizi ya Tanzania kushiriki mashindano ya kimataifa ya ujuzi.
Mbilinyi amesema Enabel Tanzania imeunga mkono mashindano hayo kwa kuchangia upatikanaji wa baadhi ya vifaa vinavyotumika katika warsha za mashindano, pamoja na kusaidia zawadi kwa washindi. Amesema taasisi hiyo imeingia katika makubaliano ya kutoa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazohusiana na mashindano hayo, ikiwamo utangazaji wa tukio, ununuzi wa vifaa na zawadi kwa washindi.
Kwa Enabel, ushiriki huo ni sehemu ya kuendeleza uwekezaji unaofanywa katika vijana kupitia mafunzo ya ujuzi, kwa kuwa mashindano yanawapa nafasi ya kuonesha kile walichojifunza na kujenga kujiamini katika taaluma zao.
Hivyo, WorldSkills inakuwa sehemu ya safari ya kijana kutoka kupata mafunzo, kutumia ujuzi katika kazi au kujiajiri, hadi kuweza kushindana na vijana wengine kwa viwango vya juu.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Utoaji Elimu ya Ufundi wa Enabel Tanzania, Thomas Aikaruwa, amesema taasisi hiyo kupitia mpango wa Inclusivity imeendelea kushirikiana na vyuo mbalimbali vya ufundi nchini ili kuongeza uwezo wa walimu na wanafunzi na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema ushirikiano huo unahusisha VETA Tanga, VETA Mwanza, FETA Kigoma na FETA Mwanza, ambapo umejikita katika kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi, kuboresha mitaala na kutoa vifaa vya kisasa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
Aikaruwa amesema baadhi ya walimu wamepewa mafunzo maalumu ya kuongeza uwezo wao wa kufundisha, huku vifaa vya kisasa vikiwekwa katika karakana za vyuo ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaoendana na mazingira halisi ya kazi.
“Kimsingi, ukimuuliza mwanafunzi au mwalimu wa VETA Tanga au VETA Kigoma Enabel imefanya nini, anaweza kuanza kueleza mambo mengi, kwa sababu kuna vitu vingi ambavyo vimefanyika, ikiwamo vifaa vilivyowekwa katika karakana na mafunzo kwa walimu,” amesema.
Amesema maboresho ya mitaala yamefanyika kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na elimu ya ufundi ili kuhakikisha kozi zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Kwa mujibu wa Aikaruwa, baadhi ya vijana wamepata fursa ya kupitia mafunzo ya muda mfupi na kuanza kufanya kazi baada ya kukamilisha mafunzo.
Ametoa mfano wa kijana aliyesoma kozi ya miezi mitatu na baadaye kutumia ujuzi huo kushiriki katika mashindano ya ujuzi katika eneo lake na kushika nafasi ya kwanza, hatua iliyomuwezesha kufuzu kwa mashindano ya kitaifa ya WorldSkills.
Hata hivyo, amesema thamani kubwa ya mafunzo hayo haipo kwenye mashindano pekee, bali katika uwezo ambao vijana wanaupata wa kutumia ujuzi wao katika maisha ya kila siku, kupata ajira au kuanzisha shughuli zao wenyewe.
Aidha, Enabel Tanzania imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kujenga uwezo wa vyuo vya ufundi kupitia makubaliano rasmi ya ushirikiano, yakilenga kuviwezesha vyuo kufikia hadhi ya Centre of Occupational Skills Excellence.
Aikaruwa amesema lengo ni kuhakikisha vyuo vya ufundi vinakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa mafunzo yenye ubora na yanayoendana na mahitaji ya soko, hivyo kuwaandaa vijana kuwa na uwezo wa kushindana katika ajira na pia kujiajiri.
Amesema uwekezaji katika elimu ya ufundi unapaswa kuonekana kama njia ya kumwezesha kijana kujenga maisha yake kupitia ujuzi alionao.
Amesema ushiriki wa vijana katika mashindano ya WorldSkills ni sehemu ya kuonesha kiwango cha ujuzi wanaoupata, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha mafunzo hayo yanawasaidia vijana kupata ajira, kujiajiri na kuongeza kipato.
Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanafanyika Agosti 15 hadi 24 mwaka huu katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.

More Stories
Watumishi wawili wafutwa kazi kwa utovu wa nidhamu
Kamati yapongeza WRRB, yataka WRS itumike kwa parachichi
Yas Fiber yazindua huduma Dodoma