
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya limepitisha kwa kauli moja uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi wawili wa Halmashauri hiyo kwa utovu wa nidhamu.
Akitoa taarifa hiyo Agosti 20, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, Aida Haule, amesema baraza hilo limejiridhisha kuwa taratibu zote za kiutumishi zilifuatwa kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.
Amesema watumishi hao walikuwa miongoni mwa waliokiuka miongozo na taratibu za utumishi, ikiwemo utoro wa muda mrefu kazini.
“Leo tumefanya kikao chetu cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne. Baraza hili linaendeshwa kwa taratibu, miongozo na sheria. Kuna watumishi mbalimbali wanakiuka miongozo, na sisi kama wawakilishi wa wananchi hatutamani kuona watumishi wanaondolewa kazini,” amesema.
Aida amesema Halmashauri ilifanya jitihada mbalimbali za kuwashawishi watumishi hao kurejea kazini, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.
Amesema baada ya taratibu zote kukamilika na kushindikana kwa jitihada za kuwafanya warejee kazini, baraza liliridhia kufukuzwa kwao.
“Hatutamani kuona vijana wanaondolewa kazini kwa sababu wazazi wamewasomesha na umri wao bado ni mdogo, lakini hakuna budi kuchukua hatua pale sababu zinazotolewa hazina mashiko,” amesema.
Kwa mujibu wa Aida, mmoja wa watumishi hao alieleza kuwa hawezi kuendelea na kazi kwa sababu ameolewa na mume wake hataki afanye kazi.
Ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wa Serikali wanaopata nafasi za ajira kuzitumia ipasavyo na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
“Nitoe wito kwa watumishi wa Serikali, mnapopata nafasi mzitumie na kuzitendea haki, kwani kuna watu wapo nje hawana kazi na wanatamani kupata kazi lakini hawapati fursa,” amesema.


More Stories
Ujuzi wa Wezesha Binti wawasaidia vijana kujiajiri na kupata ajira
Kamati yapongeza WRRB, yataka WRS itumike kwa parachichi
Yas Fiber yazindua huduma Dodoma