August 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya Algeria kuwekeza viwanda vya korosho Tanzania

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya ubanguaji wa korosho ya Sarl Anacard’Or ya Algeria inatarajia kutanua uwekezaji wake kwa kujenga viwanda vitatu nchini Tanzania ili kuongeza zaidi faida yake katika soko la dunia.

Akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Algeria,Mobhare Matinyi, wakati wa ziara yake kwenye kiwanda cha korosho cha kampuni hiyo jijini Oran, mmiliki na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo,Walid Dib, ameelezea mpango wake wa kuwekeza viwanda vitatu vya kisasa vya ubanguaji wa korosho nchini ili kufaidika na fursa ya korosho ya Tanzania inayosifika kwa ubora wake duniani.

“Korosho ya Tanzania ina ubora wa kipekee na tumeamua tujenge viwanda vitatu tukianzia na cha Masasi mkoani Mtwara kitakachotumia mashine za kisasa kutoka Vietnam,” amesema Dib ambaye tayari kwa kushirikiana na mbia wa ndani anakamilisha usajili wa kampuni ya kwanza itakayoitwa Kilimanjaro Nuts Limited.

Akimpongeza Dib kwa kuanza mchakato wa uwekezaji nchini Tanzania, Balozi Matinyi alimuahidi kwamba serikali itampatia ushirikiano wote anaohitaji ili atimize ndoto yake ambayo itaongeza ajira na mapato kwa serikali pamoja na kuleta ujuzi zaidi na fedha za kigeni nchini.

“Ni nia ya serikali kuhakikisha kuwa uwekezaji wa viwanda vya ubanguaji unaongezeka nchini ili kulipa thamani zaidi zao hili kabla ya kuuzwa nje na kupunguza uuzaji wa korosho ambazo hazijabanguliwa,”amesema Balozi Matinyi. 

Dib ameongeza zaidi kwamba hivi sasa anaandaa maghala ya kuhifadhia korosho wilayani Masasi mkoani Mtwara, na mwezi Septemba ataagiza mashine kutoka Vietnam ambazo zitawasili nchini na wataalamu wa kuwapa mafunzo wenzao wa Tanzania kuanzia mwezi Januari 2027. 

Akielezea mafanikio yake ya kuagiza korosho ya Tanzania,Dib amemwonesha Balozi Matinyi korosho za Tanzania zilizopitia hatua 11 za uzalishaji kiwandani hapo hadi kufungashwa na kuwa tayari kwa mauzo, akisisitiza kwamba sasa ameamua kununua korosho za Tanzania pekee. 

“Nilipokea makontena sita mwezi uliopita; sasa hivi nina mengine sita bandarini Oran huku saba yakiwa njiani baharini na mengine saba bandarini Dar es Salaam yakisubiri kuanza safari, na kila kontena limebeba tani 27 za korosho,” Amesema Dib.

Akihitimisha ziara yake kiwandani hapo, Balozi Matinyi amesema juhudi za serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), zimefanikisha uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani 617,683 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2025/26 zilizoingiza Shilingi trilioni 1.25 na kuifanya Tanzania iendelee kuwa moja ya wazalishaji wakubwa duniani baada ya Cote d’Ivoire, Vietnam na India.