Na Joyce Kasiki, Tanga
TEKNOLOJIA bunifu inayolenga kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, hususan wasioona, imeibua fursa mpya za kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi, kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika matumizi ya teknolojia.
Bunifu hiyo yenye jina iREN ulioanzishwa na kampuni ya Porto , unawawezesha walimu kuweka maudhui ya masomo, maswali na mitihani, huku wanafunzi wakiyapata kupitia vifaa maalumu vilivyoundwa kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wasioona.
Akizungumza katika banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH ) kwenye maonyesho Kitaifa ya wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu Usagara jijini Tanga kuhusu bunifu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa kampuni ya Porto ,Philbert Shio, amesema mfumo huo umeundwa kuimarisha mawasiliano kati ya walimu na wanafunzi na kupanua fursa za kujifunza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Mfumo wetu unatumika kwa ajili ya walimu pamoja na wanafunzi, ambapo wanaweza kuwasiliana moja kwa moja,walimu wanaweza kuweka maudhui mbalimbali ya masomo yote, maswali pamoja na mitihani,” amesema.
Amesema kupitia vifaa hivyo, wanafunzi wasioona wanaweza kupata maudhui ya masomo kwa njia ya kusikiliza na kushika, jambo analosema linawawezesha kujifunza kwa urahisi na kwa muda unaowafaa.
Shio amesema mfumo huo pia unampa mwanafunzi uwezo wa kuandaa kazi zake na kuwasiliana na wengine kupitia barua pepe, ikiwamo kutuma nyaraka na makala alizoandaa.
Kwa mujibu wa Shio, teknolojia hiyo inapatikana kwa Kiswahili na Kiingereza, hivyo wanafunzi wanaweza kuitumia kulingana na lugha inayotumika katika shule zao.
Amesema matumizi ya mfumo huo yanaweza pia kupunguza utegemezi wa wanafunzi kwa watu wengine katika mchakato wa kujifunza, huku yakimsaidia mwalimu kutumia muda wake kwa ufanisi zaidi.
“Teknolojia yetu inampa urahisi mwanafunzi kuweza kujitegemea na kujifunza wakati wote anapotaka. Mwalimu pia anaweza kufundisha popote pale anapotaka kwa sababu mfumo wetu unatumia intaneti,” amesema.
Ushirikiano wa wadau wahitajika
Shio amesema mafanikio ya teknolojia hiyo yanategemea ushirikiano wa serikali, taasisi za elimu, shule, watendaji wa serikali, wizara na kampuni za sekta ya mawasiliano.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza teknolojia hiyo, kuifikisha kwa wanafunzi wengi zaidi na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata fursa ya kuitumia kwa ufanisi.
“Katika shughuli zetu tunalenga kushirikiana na wadau mbalimbali. Tunaweza kutofautisha maeneo ambayo yanahitaji ushirikiano, kuanzia taasisi mbalimbali, shule, serikali na watendaji wa serikali, wizara, pamoja na makampuni mengine, hususan katika sekta ya mawasiliano,” amesema.
Ameongeza kuwa upatikanaji mpana wa teknolojia hizo unaweza kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika kupata na kutumia nyenzo za elimu.
Kwa upande wake, Alexina Masesa , mwalimu wa wanafunzi wasioona anayefundisha katika shule ya msingi yenye wanafunzi wenye ulemavu wa macho Zanzibar, amesema teknolojia ya maandishi ya Frakta iliyobuniwa kwa ajili ya watu wasioona inaweza kuongeza ufanisi katika ujifunzaji na kuwasaidia wanafunzi kufahamu teknolojia kwa undani zaidi.
Amesema teknolojia hiyo ni muhimu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho kwa kuwa inawawezesha kufahamu matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazohusiana na mashine, ikiwamo vifaa vya kuchapisha.
“Teknolojia ni nzuri, inasaidia wanafunzi kuifahamu teknolojia ya macho na aina mbalimbali za mashine, kama vile skana na printer. Inaongeza uwezo kwa wasioona kuifahamu teknolojia ya Frakta,” amesema.
Amesema teknolojia hiyo pia inaweza kuwajengea wanafunzi uelewa wa matumizi ya kompyuta na kuwasaidia kutumia vifaa vya kiteknolojia kwa ufanisi zaidi.
“Wanafunzi hiyo teknolojia itaongeza ufanisi katika masomo na pia kuongeza ubunifu na kufahamu teknolojia kwa undani zaidi,” amesema.
Alexina amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika bunifu zinazolenga watu wenye ulemavu wa macho ili kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma.
Kwa ujumla, bunifu hiyo inaonesha namna sayansi na teknolojia zinavyoweza kutumika kuvuka vikwazo vinavyowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum, huku ikifungua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa kuunganisha wabunifu, serikali, taasisi za elimu na sekta binafsi katika kujenga elimu jumuishi inayomuwezesha kila mwanafunzi kujifunza na kujitegemea.

More Stories
Kampuni ya Algeria kuwekeza viwanda vya korosho Tanzania
Nombo: Tanzania yaandaa vijana kushindana kimataifa
Diplomasia ya Uchumi Kuimarisha Nafasi Tanzania Kiuchumi