August 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diplomasia ya Uchumi Kuimarisha Nafasi Tanzania Kiuchumi



Na Joyce Kasiki, Tanga


AFISA Uhusiano Mwandamizi kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR), Maryciana Mhagama, amesema Diplomasia ya Uchumi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalenga kuimarisha nafasi ya nchi katika uchumi wa dunia kwa kutumia fursa zinazotokana na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa, hususan maeneo huru ya biashara barani Afrika.


Mhagama ameyasema hayo katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga, ambako CFR ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Amesema Tanzania inaendelea kutumia uhusiano wake wa kimataifa kukuza diplomasia ya uchumi, uwekezaji, biashara, mikutano, utamaduni na utalii.


“Pamoja na mambo mengine, Uhusiano wa Kimataifa umeweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Uwekezaji, ukuaji wa Biashara, Mikutano, Utamaduni na Utalii. Kwa kuzingatia fursa zilizopo, Tanzania inaendeleza Diplomasia ya Uchumi katika Uhusiano wa Uwili, Kikanda na Kimataifa,” amesema Mhagama.


Akizungumzia mafunzo yanayotolewa na CFR, Mhagama amesema Kituo hicho kinaendelea kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa mahiri na wenye weledi kitaaluma, wazalendo na raia wema wenye utayari wa kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa.


Amesema CFR inatoa mafunzo na kozi mbalimbali katika maeneo ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Kimkakati na Diplomasia ya Uchumi.


Aidha, amesema Kituo hicho kimeandaa mafunzo kuhusu Diplomasia, Itifaki na Ustaarabu (Diplomacy, Protocol and Etiquette), yatakayofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, katika ofisi za CFR, Dar es Salaam.


Amewataka wadau kutoka taasisi za umma na sekta binafsi kutumia fursa hiyo kujiendeleza na kuongeza ujuzi katika maeneo hayo.


Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, yenye kaulimbiu “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaendelea hadi Agosti 24, 2026.