August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM yatambuliwa kwa Machapisho Bora



Na Joyce Kasiki, Tanga


CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimepata mafanikio katika utafiti na uchapishaji wa kazi za kitaaluma baada ya watafiti wake zaidi ya 14 kutunukiwa tuzo kwa machapisho yao yaliyochapishwa katika majarida ya kimataifa yenye hadhi kubwa.


Tuzo hizo zilikabidhiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.


Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayesimamia Utafiti, Profesa Nelson Boniface akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu jijini Tanga, amesema mafanikio hayo yanaonyesha ubora wa tafiti zinazofanywa na watafiti wa chuo hicho.


Amesema asilimia 52 ya machapisho ya UDSM yanaonekana katika majarida ya kimataifa yenye viwango vya juu, yakiwemo ya kundi la Q1, pamoja na machapisho yanayotambuliwa na mifumo ya Web of Science na Scopus.


Kwa mujibu wa Profesa Boniface, baadhi ya tafiti hizo zimechapishwa na wachapishaji wakubwa wa kimataifa, akitaja Elsevier, huku idadi ya machapisho katika majarida hayo ikiongezeka kwa asilimia 16.


Amesema tafiti zilizotunukiwa zimehusisha nyanja mbalimbali, zikiwemo afya, hisabati, fizikia na uhandisi, huku zikilenga kuzalisha maarifa na suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii na sekta mbalimbali.


Profesa Boniface amesema kutambuliwa kwa watafiti hao ni uthibitisho wa mchango wa UDSM katika kuzalisha maarifa yenye viwango vya kimataifa.


Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya UDSM katika tafiti zinazolenga kuchochea maendeleo, hasa katika maeneo ya afya, sayansi asilia, biolojia na uhandisi.