Na Joyce Kasiki,Timesmajiraonline,Tanga
NAIBU Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Razack Lokina, amesema chuo hicho kinaendelea kuwekeza katika utafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na Taifa kwa ujumla.
Profesa Lokina amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la UDOM kwenye Maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika Usagara, mkoani Tanga.
Amesema UDOM imeshiriki maonyesho hayo kwa lengo la kuonesha matokeo ya tafiti na ubunifu unaofanywa na wanafunzi na wataalamu wa chuo hicho, huku akieleza kuwa baadhi ya bunifu hizo zimejikita katika maeneo muhimu yakiwemo kilimo, afya na lishe.
“Tumekuja Tanga kwa ajili ya maonesho ya ubunifu na sayansi, ambapo vyuo vikuu vinaonesha kazi mbalimbali zinazofanywa na watafiti na wanafunzi,” amesema Profesa Lokina.
Ameeleza kuwa katika sekta ya kilimo, UDOM inaendelea kufanya tafiti zinazolenga kuongeza tija na kusaidia jamii kutumia teknolojia na maarifa yanayopatikana kupitia tafiti hizo, pamoja na kuwasaidia wakulima kupata thamani zaidi kutokana na mazao yao.
Katika eneo la afya, Profesa Lokina amesema UDOM imefanya utafiti unaohusu lishe kwa wagonjwa wenye magonjwa ya figo na moyo, ambapo utafiti umebaini kuwa baadhi ya vyakula maalumu vinaweza kuwa na manufaa zaidi kwa wagonjwa hao kuliko kutegemea vyakula vya kawaida vya nyumbani.
Amesema bunifu na tafiti hizo zinaonesha umuhimu wa vyuo vikuu kushirikiana na jamii katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
“Tunapaswa kuja kwenye maonesho kama haya na kujifunza, kwa sababu kuna mambo mengi yanayoweza kutumika kutatua changamoto nyingi zinazoisumbua nchi,” amesema.
Kwa upande wa fursa za elimu, Profesa Lokina amesema UDOM imeanzisha programu mpya katika ngazi ya shahada ya kwanza na uzamili, huku akiwataka vijana ambao hawakuweza kuomba nafasi katika awamu ya kwanza kutumia fursa hiyo wakati dirisha la pili la udahili litakapofunguliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Amesema dirisha hilo pia litawapa nafasi waombaji ambao hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza au wanaotaka kubadili programu walizoomba awali.

More Stories
Kamati ya Bunge Yapokea Taarifa ya AFCON 2027
Elimu, Utafiti, Ujuzi, Ubunifu kujenga Tanzania imara
Dkt.Lingwanda apongeza ubunifu wa vijana katika maonesho ya NACTVET