Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
SHIRIKA la Posta Tanzania kupitia huduma ya EMS kufuatia maboresho ambayo limefanya limepunguza muda wa kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi ikiwemo Marekani, Canada na Ufaransa.
Ambapo awali shirika hilo lilikuwa likitumia kati ya siku saba hadi 10 kusafirisha mizigo lakini sasa linatimia kati ya siku tatu hadi tano, huku likishusha gharama na kutoa punguzo maalumu kwa wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mkoa wa Mwanza.
Meneja wa Huduma za EMS wa Shirika la Posta Tanzania Ahmad Rashid amezungumza hayo Agosti 17,2026 mkoani Mwanza mbele ya waandishi wa habari,ambapo amesema,maboresho hayo yamelenga kuwawezesha wananchi kupata huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa haraka,usalama,uhakika na gharama nafuu ndani na nje ya nchi.
Amesema changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo iliyokuwepo awali imepungua baada ya shirika hilo kuongeza magari 28 mapya ya ukubwa tofauti kati ya Januari na Juni mwaka huu,hatua iliyoongeza uwezo wa kusafirisha mizigo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Rashid amesema,shirika limeongeza wasafirishaji wa kimataifa kutoka wawili hadi sita na kuimarisha ushirikiano na mashirika makubwa ya ndege, huku mizigo katika mikoa mikubwa inafika ndani ya saa 24,na kwa sasa EMS inatoa huduma katika nchi 88, huku Tanzania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani wenye nchi wanachama 192, hivyo kuwezesha kufikisha mizigo katika nchi nyingine kupitia ushirikiano wa kimataifa.
“Tumekuja na mfumo wa “we pick, we pack and we deliver”, unaowezesha shirika kufuata mzigo alipo mteja, kuufungasha na kuusafirisha hadi kwa mpokeaji, hatua inayorahisisha huduma kwa wananchi,”amesema Rashid.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Philip Kowero amesema,EMS ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupunguza gharama za usafirishaji na kuwawezesha wananchi kupata fursa za masoko ya kimataifa.
Kowero amesema,Mwanza ni kitovu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa,hivyo huduma hiyo itawarahisishia wananchi kusafirisha bidhaa mbalimbali ikiwemo samaki,dagaa na mazao mengine kutoka Ziwa Victoria kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema,shirika limetoa punguzo maalumu kwa wananchi wa Mwanza wanaotuma mizigo kwenda Marekani,Canada na Ufaransa huku muda wa kufikisha mizigo ukiwa siku tatu hadi tano,kutegemea taratibu za forodha.
Hivyo amesema,maboresho hayo yamezingatia usalama wa mizigo, vifurushi na nyaraka za wateja,huku shirika likishirikiana na kampuni zaidi ya sita za usafirishaji wa kimataifa kuhakikisha mizigo inafika kwa wakati na salama.
Aidha amesema,shirika limeboresha huduma zake kidigitali kwa kutumia programu ya “Posta Kiganjani”,inayomwezesha mteja kujisajili,kuagiza huduma na kupata huduma za EMS bila kufika katika ofisi za Posta, huku mfumo wa “track and trace” ukimwezesha kufuatilia mzigo wake.
Kowero amesema,maboresho hayo yanalenga kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mwanza kupanua masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi, kukuza biashara na kuchangia ongezeko la Pato la Taifa.

More Stories
Masandawana Fc yajinyakulia mil.10/- Tulia Trust Uyole Cup 2026
Maji salama ya wafikia wakazi 22,482
Masenza Mwenyekiti JUWAKITA Mwanza