August 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maji salama ya wafikia wakazi 22,482

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Misungwi

WAKAZI zaidi ya 22,482 wa vijiji vya Ng’ombe,Iteja,Mbela B,Mbela D,Mbela C, Old Misungwi,Mwamanga na Mitindo B, wilayani Misungwi mkoani Mwanza wameondokana na adha ya kufuata maji umbali mrefu na yasiyo salama iliowakumba kwa muda mrefu.

Hii ni baada ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi Misungwi Mjini uliogharimu kiasi cha sh.milioni 888 ambao umefikia asilimia 99.5 ya utekekalezaji wake kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru wilayani humo.

Wakizungumzia wakati wa uzinduzi huo Agosti 16,2026,baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wameeleza namna ambavyo walilazimika kuamka usiku kwa ajili ya kutafuta maji kwa umbali mrefu hali ilisababisha kutumia muda mwingi katika jambo hilo na kuacha shughuli nyingine ikiwemo za kiuchumi.

“Tulikuwa tunaamka usiku kufuata maji mbali na wakati mwingine kwenye madibwi ambayo yalikuwa ni machafu na siyo salama kwa afya yetu, hivyo tulilazimika kuacha shughuli nyingine za maendeleo.Lakini kwa sasa tunapata maji kwa urahisi kwani mabomba yapo katika miji ya watu,”amesema Maria Shija mmoja wa wananchi wa Misungwi.

Naye Musa Joseph amesema,wananchi wa maeneo hayo hususani wanawake walikuwa wanaamka saa kumi usiku kwa ajili ya kufuata maji hali iliotishia ndoa kwani kuna muda wanaume walikuwa wanapata wasiwasi na kuhoji kama wake zao walikuwa wanaenda kwenye maji au kulikuwa na vitu vingine vinaendelea.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang’onda,Msimamizi wa Miradi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),Mhandisi Nuhu Said amesema,mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi Misungwi,uliibuliwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mji wa Misungwi.

Ambapo lengo kuu la mradi huo ni kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika mji wa Misungwi,unatekelezwa kupitia mkataba Na. ΑΕ/042/2021-2022/W/43 chini ya Mkandarasi DATTI CONSTRUCTION LTD kwa usimamizi wa MWAUWASA huku ujenzi ilianza Oktoba 2,2023 na hadi Februari 9,2026 na kwa sasa unatoa huduma.

Mhandisi Said amesema,mradi huo umegharimu kiasi cha sh.milioni 888 na ukihusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na choteo la maji lenye ujazo wa lita 50,000,ujenzi wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 150,000 na 90,000,ununuzi na ufungaji wa pampu mbili zenye uwezo wa kuzalisha lita 50,000 kwa saa, ufungaji wa transformer KV 100,ulazaji wa mabomba ya HDPE PN 16 (mm 160 na 110) umbali wa km 3.5, ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na chemba 10 za kuhifadhi valves.

“Mradi huu umenufaisha wakazi zaidi ya 22,482 wa vjiji vya Ng’ombe,Iteja,Mbela B,Mbela D,Mbela C,Old Misungwi, Mwamanga na Mitindo B. Upatikanaji wa huduma za maji katika Mji wa Misungwi na Vijiji vya jirani umeongezeka kutoka asilimia 90 hadi asilimia 97,hivyo kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu na kumtua mama ndoo kichwani,”amesema Mhandisi Said.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang’onda,amewasisitiza wananchi umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji na kutumia huduma hiyo kwa ufanisi ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unadumu na kuendelea kunufaisha jamii.

Hata hivyo uzinduzi wa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada endelevu za Serikali kupitia Wizara ya Maji katika kuboresha huduma muhimu ya maji kwa wananchi.