August 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANTRADE yashiriki hafla ya ufungaji wa maonesho ya 10 ya Wakulima Zanzibar

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika hafla ya ufungaji rasmi wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Zanzibar, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Kilimo wa Zanzibar,
Suleiman Masoud Makame.

Katika hotuba yake, Waziri wa Kilimo ametoa maelekezo mbalimbali yenye lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko kwa wakulima.

Vilevile, Waziri amezipongeza taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo TanTrade, kwa kushiriki katika maonesho haya kwa Miaka kumi mfululizo, akieleza kuwa mchango wake umeongeza mvuto na pia kufanya maonesho ya mwaka huu kuwa makubwa na bora zaidi ikilinganishwa na miaka iliopita.

Katika maonesho hayo, TanTrade imeshiriki kikamilifu kwa kutoa elimu na taarifa kwa wananchi, wafanyabiashara na wazalishaji kutoka sekta mbalimbali, ikiwemo Kilimo na Uvuvi, kuhusu fursa za biashara, masoko na huduma zinazotolewa na Mamlaka.

Kupitia banda lake, TanTrade pia imewafikia wananchi wengi kwa kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yake, ikiwemo kuwezesha na kuratibu ushiriki wa wafanyabiashara katika maonesho, pamoja na umuhimu wa kutumia Nembo ya Taifa ya “Made in Tanzania.”

Elimu hiyo imelenga kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kutambua namna Nembo ya “Made in Tanzania” inavyosaidia kutambulisha bidhaa za Tanzania, kuongeza uaminifu wa watumiaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa na kufungua fursa za kuingia katika masoko ya ndani na ya kimataifa.