Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
SERIKALI imeeleza kuwa ujenzi wa Kituo Kipya cha Saratani Mbeya utakuwa hatua muhimu katika kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi za saratani karibu na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 15, 2026, na Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Saratani Jijini Mbeya.
Dkt.Nyembea amesema saratani imeendelea kuwa changamoto kubwa duniani, huku takwimu za mwaka 2024 zikionyesha kuwa takribani watu milioni 20 waligundulika kuwa na ugonjwa huo duniani, ambapo milioni 9.7 walipoteza maisha.
Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani takribani 45,000 kwa mwaka, huku karibu 30,000 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.

“Sasa ukija katika nchi yetu tuna wagonjwa 45,000 ambao wanagundulika na saratani na kati ya hao 30,000 wanafariki kila mmoja tunampoteza kwa sababu ya saratani Takribani asilimia 50 ya saratani zinaweza kuzuilika na nyingine zinaweza kugundulika mapema,” amesema.
Amesema serikali imeamua kuwekeza katika upanuzi wa huduma za saratani pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili kuongeza uwezekano wa wagonjwa kugundulika na kutibiwa katika hatua za awali.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyembea, uwepo wa vituo vya kikanda, ikiwamo Mbeya, utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza mzigo wa wagonjwa kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kupata matibabu.
Amesema kituo kingine cha saratani kinatarajiwa kuanza kujengwa Arusha mwezi Oktoba mwaka huu, huku mipango ikiendelea kwa ajili ya kujenga vituo vingine Kigoma na Mtwara.

“Tunapokuwa na vituo vya kikanda kama Mbeya, na kingine kitaanza kujengwa Arusha kuanzia mwezi Oktoba, pamoja na Kigoma na Mtwara, vyote hivyo vitaweza kusaidia kudhibiti na kuponya watu wengi ambao watakuwa wanagundulika katika hatua za awali,” amesema.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibobezi katika Kanda mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa awali huduma jumuishi za saratani zilikuwa zikitegemea zaidi Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, kabla ya huduma hizo kupanuliwa hadi Kanda ya Ziwa kupitia Hospitali ya Bugando.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo, amesema ujenzi wa vituo vya kikanda ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupanua huduma za saratani nchini.
Amesema katika mkakati wa serikali wa kupambana na saratani wa mwaka 2012 wa kipindi cha miaka 10, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ilipewa jukumu la kusambaza huduma za kibingwa na kibobezi za saratani katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema serikali imewekeza zaidi ya bil.60 kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika kuboresha miundombinu ya huduma za saratani.
Kuhusu Kituo cha Saratani Mbeya, amesema serikali imewekeza takribani Sh11 bilioni katika ujenzi wa mradi huo, ambao unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari 2027 ili wananchi waanze kupata huduma.
Dkt. Msemo amesema kituo hicho pia kina fursa ya kukuza utalii wa tiba, hasa kwa wagonjwa kutoka nchi jirani kama Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambao sasa wanaweza kupata huduma Mbeya badala ya kusafiri hadi Ocean Road.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo, Ally Mtigita, amesema ujenzi ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.
Amesema mradi huo una thamani ya takribani Sh10.4 bilioni na hadi sasa umefikia asilimia 57 ya utekelezaji.
Amesema kazi zinaendelea kwa kasi kuhakikisha kituo hicho kinakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kituo hicho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa miundombinu muhimu ya afya katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi, tiba na ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani karibu na maeneo wanayoishi.

More Stories
Waziri Kabudi:Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Lukuvi
Mkenda:Ujuzi agenda kuchochea ajira kwa vijana
Zimebaki siku sita uzinduzi wa JNHPP