Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Ufaransa
WAKATI Dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia jana, Serengeti Breweries Limited (SBL) inaungana na maadhimisho hayo kwa namna ya kipekee baada ya bidhaa zake kuthibitika kuwa na viwango vya kimataifa.
Mafanikio hayo yamekuja kufuatia Serengeti Lite, Serengeti Lager na Serengeti Lemon kutunukiwa Tuzo za Gold Quality Awards 2026 kutoka taasisi maarufu duniani ya Monde Selection.
Tuzo za Gold Quality Awards zinazotolewa na Monde Selection, hutolewa kwa bidhaa zinazokidhi viwango vya juu vya ubora vinavyotambulika kimataifa baada ya kupitia mchakato makini wa tathmini unaofanywa na jopo huru la wataalamu wa kimataifa. Bidhaa hupimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa jumla, ladha, mwonekano, ubunifu, taarifa kwa watumiaji pamoja na uzoefu wa mtumiaji, ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotambulika duniani.
Imeelezwa kuwa, Monde Selection ilianzishwa mwaka 1961 mjini Brussels, Ubeligiji, ikiwa ni taasisi huru ya kimataifa inayojihusisha na tathmini ya ubora wa bidhaa za walaji zaidi ya miaka 65, taasisi hiyo imekuwa ikitathmini maelfu ya bidhaa katika makundi mbalimbali, ikiwemo vyakula, bia, vinywaji vikali, bidhaa za afya na lishe pamoja na vipodozi.

Mafanikio haya yanaakisi dhamira endelevu ya Kampuni ya Serengeti ya kuzalisha vinywaji vya ubora wa kiwango cha kimataifa kupitia uwekezaji unaoendelea katika teknolojia za kisasa za uzalishaji, mifumo madhubuti ya uhakiki wa ubora, pamoja na ubunifu unaomweka mlaji katika kitovu cha kila hatua ya shughuli zake.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Ugavi wa SBL Joseph Cheloti, alisema tuzo hizo ni uthibitisho wa dhamira kuu ya kampuni katika kuhakikisha bidhaa zake zinadumisha viwango vya juu vya ubora.
“Kupokea Tuzo za Gold Quality Awards kutoka Monde Selection ni heshima kubwa na uthibitisho kuwa bidhaa zetu zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa. Tunajivunia mafanikio haya ambayo yanadhihirisha kujitolea kwa wafanyakazi wetu, ubora wa malighafi tunazotumia pamoja na uimara wa mifumo yetu ya uzalishaji. Zaidi ya yote, tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na kutuunga mkono”, alisema Cheloti.
Aliongeza kuwa, kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na maendeleo ya bidhaa ili kuhakikisha watumiaji nchini Tanzania na katika masoko mengine wanaendelea kupata vinywaji vinavyokidhi viwango vya juu vya ubora duniani.

Mbali na bidhaa hizo tatu za bia, chapa ya vinywaji vikali ya kampuni hiyo, TZEE, pia ilitunukiwa Tuzo ya Gold Quality Award 2026. Kupokea Tuzo nne za Gold Quality Awards kwa wakati mmoja kunazidi kuimarisha nafasi ya Kampuni hiyo, kama miongoni mwa wazalishaji wa vinywaji wanaozingatia ubora unaotambulika kimataifa, huku ikiendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania na kuonesha ubora wa bidhaa zake katika jukwaa la dunia.

More Stories
Nyerere:Asasi wekeni mipango yenu kuoanisha na Dira 2050
Kabudi aagiza ujenzi wa Ofisi kukamilika kwa wakati
Serikali yakabidhi Pampu 52 za umwagiliaji kwa wakulima