August 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima Kanda ya Kati wavuna na Mixx

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKULIMA wa Kanda ya Kati wanaotumia huduma za kifedha za Mixx by Yas kupitia vyama vya ushirika wameendelea kunufaika na malipo ya kidijitali na zawadi mbalimbali, hatua inayotajwa kuongeza usalama wa fedha, kuharakisha malipo na kuhamasisha uzalishaji wa mazao.

Akizungumza katika hafla ya Vuna na Mixx iliyofanyika wakati wa Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema ushirikiano kati ya Tume na Mixx umeleta mageuzi katika mfumo wa malipo kwa wakulima wanaouza mazao kupitia stakabadhi za ghala.

Amesema, matumizi ya malipo ya kidijitali yameondoa changamoto zilizokuwa zikitokana na matumizi ya fedha taslimu, ikiwemo ucheleweshaji wa malipo na upotevu wa fedha, huku wakulima wakipokea fedha zao kwa usalama na kwa wakati.

“Malipo yanapowafikia wakulima kwa wakati yanawapa motisha ya kuongeza uzalishaji. Tumeona mabadiliko makubwa katika mfumo wa ushirika na ongezeko la mazao kutokana na kuimarika kwa huduma hizi,” amesema Dkt. Ndiege.

Amewataka wakulima wanaonufaika na mfumo huo kuwa mabalozi wa matumizi ya huduma za kidijitali ili kuwahamasisha wenzao kujiunga na mfumo huo, huku akiwapongeza maafisa ushirika na viongozi wa AMCOS kwa kuendelea kutoa elimu inayowasaidia wakulima kutumia huduma hizo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa Mixx Kanda ya Kati,  Charles Gasper, amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali na vyama vya ushirika kuhakikisha wakulima wanapata huduma za kifedha zilizo salama, rahisi na za haraka.

Amesema, katika hafla hiyo Mixx iliwatunuku zawadi wakulima zaidi ya 25 kutoka Kanda ya Kati waliotumia huduma zake kupitia vyama vya ushirika, zikiwemo pikipiki, maguta na baiskeli, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.

“Tunaamini tukimwezesha mkulima, tunachangia ukuaji wa familia yake, jamii na uchumi wa taifa. Hivyo tutaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo kuhakikisha wakulima wengi zaidi wananufaika na huduma za Mixx,” amesema Gasper.