August 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bima ya mazao kuwa kinga kwa wakulima

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

SHIRIKA la Taifa la Bima (NIC) limewataka wakulima na wafugaji nchini kutumia bima kama kinga ya shughuli zao za uzalishaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame, mafuriko na majanga mengine ya asili.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu zaidi katika kipindi ambacho mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kufanya misimu ya kilimo kutotabirika, huku wakulima katika Nyanda za Juu Kusini wakikabiliwa na matukio ya mafuriko na mvua za mawe yanayoweza kuharibu mazao na kuathiri kipato cha kaya.

Afisa Bima wa NIC, Tawi la Sumbawanga, Pili Salum, amesema bima ya mazao inalenga kumlinda mkulima dhidi ya hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na changamoto mbalimbali za uzalishaji, zikiwemo ukame, mafuriko, wadudu waharibifu na magonjwa.

Amesema katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, mafuriko na mvua za mawe ni miongoni mwa majanga yanayoweza kusababisha hasara kubwa kwa wakulima, hali inayofanya ulinzi wa kifedha kupitia bima kuwa muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Salum, mazao yanayoweza kukatiwa bima ni pamoja na pamba, korosho, kahawa, tumbaku, maharage, mahindi, mpunga, shayiri, alizeti na chai.

Mbali na mazao, amesema NIC pia inatoa bima ya mifugo inayomlinda mfugaji dhidi ya hasara inayoweza kutokana na vifo vya mifugo vinavyosababishwa na ajali, magonjwa au wizi.

Amesema bima hiyo pia inaweza kumsaidia mfugaji kupata dhamana katika taasisi za kifedha, hivyo kumpa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za ufugaji.

Salum amewahimiza wakulima na wafugaji kutumia fursa zinazotolewa na NIC kwa kukatia bima shughuli zao, akisisitiza kuwa bima ni nyenzo muhimu ya kujenga ustahimilivu wa sekta ya kilimo na mifugo dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Salum ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kilele cha Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa wakulima kutoka Wilaya ya Mbarali, Juma Abdalah, amesema baadhi ya wakulima wameanza kuwa na mwamko wa kutumia bima kutokana na kutambua umuhimu wake katika shughuli zao za kilimo.

“Wengi wetu tumekuwa tukitoa mkazo kwenye suala la bima, ingawa baadhi yetu bado tuna uelewa mdogo. Tunaendelea kuelimishana ili wote tuweze kwenda pamoja,” amesema.