Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kwa kiwango cha hadi shilingi milioni 7.5 endapo benki itafilisika au kufutiwa leseni.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima na wafugaji Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma,.
“Kiwango hicho kinahakikisha mteja mwenye amana zisizozidi shilingi milioni 7.5 analipwa fedha zake zote ikiwa benki yake itafungwa.”amesema Mwambande
Amesema Mfuko wa Bima ya Amana huchangiwa na benki pamoja na taasisi za fedha zinazopokea Amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila benki huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake mara moja kwa mwaka.
Mwambande amesema fedha zinazokusanywa huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wateja pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake.
Aidha, amesema kwa sasa DIB inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa kati ya mwaka 2000 na 2018 ambazo ni Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Bank, Covenant Bank for Women, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank.

More Stories
Dkt Chaya:Tagazeni mafanikio ya Kampeni ya mama Samia legal Aid
FAO yawataka wakulima kuzingatia kanuni bora za ufugaji
Wakulima waliowezeshwa na TADB waeleza mafanikio yao nanenane